Mali yajibu mapigo kwa Marekani

BAMAKO-Serikali ya Mali imetangaza kwamba, raia wa Marekani watahitajika kuweka dhamana ya visa (visa bond) ya hadi dola za Kimarekani 5,000 hadi 10,000 ikiwa watatafuta visa za biashara (B‑1) au utalii (B‑2) ili kuingia nchini Mali.

Hatua hii inakuja kama majibu ya sera ya Marekani inayoitaka Mali kuweka dhamana ya kati ya dola za Kimarekani 5,000 hadi 10,000 kwa raia wake wanaotaka visa za Marekani.

Marekani imeazimia kuanzisha mpango wa majaribio (pilot program) ambapo raia wa Mali wanapokuwa wanatafuta visa za biashara au utalii wanapaswa kuweka dhamana.

Audha,Mali imelaani uamuzi huo kama hatua inayolalia upande mmoja na ambayo inakiuka makubaliano ya ushirikiano wa visa ya muda mrefu yaliyosainiwa mwaka 2005 kati ya Mali na Marekani.

Katika taarifa rasmi,Wizara ya Mambo ya Nje ya Mali imesema, itaomba kutumia kanuni ya usawa wa pande zote (reciprocity) ambapo raia wa Marekani watapewa masharti sawa na yale yanayotolewa kwa raia wa Mali chini ya sera za Marekani.

Raia wa Marekani wanaoomba visa Mali watatakiwa kuweka dhamana sawa ikihusisha masharti na vigezo vinavyotumika kwa raia wa Mali.

Mpango wa Marekani unatakiwa kuanza kutekelezwa Oktoba 23, 2025 kwa raia wa Mali, ambapo wale walioomba visa za B‑1/B‑2 watatakiwa kuweka dhamana ya dola 5,000 au 10,000.

Dhamana hiyo itarudishwa kwa muombaji ikiwa atatimiza masharti ya kuondoka Marekani ndani ya muda uliopangwa, na hatakuwa ametumia haki za hifadhi au kupita muda wa visa.

Iwapo mtu atavunja masharti ya visa kwa mfano kukaa bila ruhusa, dhamana inaweza kukatwa au ikabaki kwa Serikali ya Marekani.

Mali imesema kuwa,sera ya Marekani ya Visa Bond ni ukiukaji wa makubaliano ya mwaka 2005 yaliyoanzisha utoaji wa visa za muda mrefu za kuingia mara nyingi kati ya nchi hizo mbili.

Katika tamko, Mali imeonesha kutoridhishwa na utendaji wa upande mmoja wa Marekani na kusema masuala kama hayo yajadiliwe kwa heshima na mazungumzo ya pande zote.

Hata hivyo, Mali inasisitiza kuwa, itaendelea kushirikiana na Marekani kwenye masuala ya kuzuia uhamiaji haramu na ushirikiano wa kiusalama, lakini kwa kuzingatia msingi wa adilifu na usawa.

Siku rasmi ya kuanza utekelezaji wa dhamana hiyo kwa raia wa Marekani bado haijatajwa wazi au kutolewa kitaifa kwa undani nchini Mali.

Pia,haijulikani jinsi Mali itashughulikia utoaji, ukaguzi, na urejeshwaji wa dhamana au ni nani atakayechagua kiwango cha dhamana, ni mbinu gani za kulipia, na masharti ya kurejesha au kukata dhamana hiyo.

Wachambuzi wa masuala ya diplomasia wanasema kuwa, hatua hiyo inaweza kusababisha mgogoro wa usafiri, ushawishi wa utalii na kuchochea migogoro ya kidiplomasia kati ya Mali na Marekani.

Pia kuna wasiwasi kwamba sera hizi za dhamana zinaweza kuleta mzigo wa kifedha kwa wasafiri wenye nia njema na kupunguza usafiri halali.

Marekani imetangaza tozo hizo mpya kwa nchi za Afrika ikiwa na lengo la kutaka kulinda mipaka yake na usalama wake.

Nchi nyingine za Afrika zilizoingizwa katika mpango wa majaribio wa mwaka mmoja unaolenga mataifa yenye kiwango kikubwa cha watu wanaokaa zaidi ya muda wa visa zao nchini  Marekani ni Gambia, Malawi, Zambia,MauritaniaTanzania, Sao Tome na Principe.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news