DAR-Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Cosato Chumi, amemwakilisha Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mohamoud Thabit Kombo, kushiriki kwenye maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya Jamhuri ya Korea yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. 

Mhe. Chumi ameipongeza Jamhuri ya Korea kwa kuadhimisha Siku ya Kitaifa ya Taifa hilo ambalo wamepiga hatua kubwa ya maendeleo kwa miaka ya hivi karibuni.
Jamhuri ya Korea inashirikiana na Tanzania kwenye miradi mbalimbali ya Uwekezaji, ujenzi wa Miundombinu, Maji, Kilimo, Afya, Uchukuzi, Madini, TEHAMA na Elimu.
Mhe. Chumi amesema, Tanzania inashukuru Serikali ya Korea kwa kusaidia ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo Daraja la Tanzanite Bridge Dar es Salaam; Malagalasi Bridge Kigoma; ukarabati wa Hospitali ya akina Mama na Watoto Chanika; kuanzisha Serengeti Media Centre na utekelezaji wa miradi jumuishi wa ufugaji wa mazao ya baharini.
Mhe. Chumi amesema kiwa Tanzania itaendelea kushirikiana zaidi na Korea ili kuimarisha ushirikiano wa uwili na kimataifa pamoja na kishirikiana kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050.
Kwa upande wake, Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini, Mhe. Ahn Eun-Ju ameeleza masuala mbalimbali ambayo Korea inashirikiana na Tanzania na kueleza dhamira ya Serikali yao kuendelea kushirikiana na nchi yetu. Amesema kuwa Korea na Tanzania zitaendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali kiutamaduni, kijamii na kiuchumi ili kuleta maendeleo baina ya nchi zetu na wanachi wao kwa ujumla.Tanzania na Korea zilianzisha ushirikiano wa Kidiplomasia tangu mwaka 1992.







