ZANZIBAR-Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amehitimisha rasmi kampeni za CCM kwa upande wa Pemba, akiwataka wananchi kukichagua chama hicho ili kiendelee kuleta maendeleo na kulinda tunu za Taifa.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 23,2025 katika mkutano wa kufunga kampeni za CCM uliofanyika Uwanja wa Michezo wa Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema kuwa CCM inastahili kuaminiwa tena kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020–2025, ambayo imeleta mafanikio makubwa katika sekta za maendeleo ikiwemo miundombinu, afya, elimu, kilimo, na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali atakayoiongoza katika awamu ijayo, baada ya kupata ridhaa ya Wazanzibari, inalenga kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwa kasi zaidi.
Ametaja baadhi ya mipango hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda katika maeneo ya Dunga, Zuze na Chamanangwe, Pemba, kwa lengo la kuongeza ajira kwa vijana na kuwawezesha wananchi kiuchumi kupitia mikopo isiyo na riba.
Aidha, ameahidi ujenzi wa barabara za lami katika barabara zote za ndani za wilaya na mikoa ya Unguja na Pemba, pamoja na kuendelea kuboresha huduma za elimu kupitia ujenzi wa skuli 20 za ghorofa na dakhalia, ambapo tayari Serikali imesaini mkataba na mkandarasi wa mradi huo.
Amesema pia Serikali itahakikisha upatikanaji wa maji safi na salama katika kila shehia, na kujenga hifadhi ya mafuta itakayowezesha upatikanaji wa mafuta kwa uhakika wakati wote.
Halikadhalika, Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa Serikali ina mpango wa kuzalisha zaidi ya ajira 350 mpya katika sekta za ualimu, afya na vikosi vya ulinzi na usalama, sambamba na kuwawezesha vijana kujiajiri wenyewe.
Kuhusu maslahi ya watumishi wa umma, amesema Serikali ijayo itapandisha mishahara kulingana na ukuaji wa uchumi, huku ikiendeleza ujenzi wa nyumba bora za bei nafuu katika kila wilaya.
Akizungumzia sekta ya usafiri wa baharini, Dkt. Mwinyi amesema Serikali italiimarisha Shirika la Meli la Zanzibar kwa kulinunulia meli mpya ili kuboresha huduma za usafiri kati ya Unguja na Pemba.













.jpg)
.jpg)