NA DIRAMAKINI
UONGOZI wa Klabu ya Yanga (Young Africans Sports Club) ya jijini Dar es Salaam umemtangaza rasmi Pedro Valdemar Soares Gonçalves raia wa Ureno, kuwa kocha mkuu mpya wa klabu hiyo.
Gonçalves ametangazwa Oktoba 25,2025 ikiwa ni siku chache zimepita baada ya Klabu ya Young Africans Sc kutangaza kuvunja mkataba wa Kocha Mkuu wa kikosi cha kwanza, Romain Folz.
Yanga SC ilivunja mkataba huo saa kadhaa baada ya klabu hiyo kupokea kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Silver Striker Fc ya Malawi kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL)
Kupitia taarifa ya Oktoba 18, 2025 iliyotolewa na uongozi wa klabu hiyo ilieleza kuwa, katika kipindi hicho kikosi hicho kilikuwa chini ya Kocha Msaidizi Patrick Mabedi hadi mchakato wa kutafuta Kocha Mkuu ulipokamilika.
Ujio wa Pedro Valdemar Soares Gonçalves ndani ya Yanga SC,ni hatua muhimu ambayo inatarajiwa kuongeza ubora wa kiufundi na ushindani wa kimataifa wa klabu hiyo kongwe barani Afrika.
Pedro Gonçalves mwenye umri wa miaka 49, ni kocha mwenye leseni ya juu ya ukocha (UEFA Pro License) kutoka Shirikisho la Soka la Ureno (FPF) na amejizolea sifa kwa kuendeleza vipaji na kuongoza timu kwa nidhamu na falsafa ya kisasa ya uchezaji.
Gonçalves alianza kazi yake ya ukocha mwaka 1996 akiwa timu ya Amora FC nchini Ureno kama msaidizi wa kocha.
Aidha,baadaye alihamia Sporting Clube de Portugal, mojawapo ya akademi maarufu barani Ulaya, ambapo alihusika moja kwa moja na malezi ya wachezaji waliokuja kuwa nyota kama William Carvalho, João Mário na Armindo Tué Na Bangna (Bruma).
Mwaka 2015,Gonçalves alihamia Angola, akichukua jukumu la kocha wa maendeleo ya vijana katika klabu ya Primeiro de Agosto.
Kazi yake nzuri ilimpa nafasi ya kuwa kocha mkuu wa timu ya vijana (U-17) ya Angola, ambayo aliipeleka FIFA U-17 World Cup 2019 kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hilo.
Kutokana na mafanikio hayo, aliteuliwa kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Angola (Palancas Negras) mwaka 2019, akiongoza timu hiyo kwa mafanikio makubwa hadi 2025.
Pedro Gonçalves anachukuliwa kuwa miongoni mwa makocha wa kizazi kipya kutoka Ureno wanaolenga mabadiliko ya mbinu na maendeleo ya wachezaji huku wakipata mafanikio bora uwanjani.
Pia,Gonçalves anatajwa kuwa ni mfano wa makocha wa Ulaya wanaoleta mabadiliko chanya katika soka la Afrika kwa kuunganisha taaluma ya kisasa na vipaji vya asili vya wachezaji wa Kiafrika.
Kupitia kazi yake Angola, aliongeza ubora wa mafunzo ya vijana na kuanzisha mfumo wa "technical transition model" unaounganisha timu za vijana na timu ya wakubwa.
Tags
Breaking News
Habari
Kocha Mkuu Yanga
Kocha Mpya Yanga SC
Michezo
Pedro Gonçalves
Pedro Valdemar Soares Gonçalves
