ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amejumuika na Walimu wa Madrasa, Masheikh pamoja na Uongozi wa Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar katika Dua Maalumu ya kumuombea yeye pamoja na kuliombea Taifa na Uchaguzi Mkuu ujao.

Dua hiyo imefanyika leo katika Ukumbi wa Dkt. Ali Mohamed Shein, Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja, na imeandaliwa na Afisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kushirikiana na Jumuiya ya Kuendeleza Walimu wa Vyuo vya Qur’an Zanzibar (JUKUWAVOQUZA).
Akizungumza katika hafla hiyo, Alhaj Dkt. Mwinyi amewakumbusha wananchi umuhimu wa kuiombea nchi amani, hasa katika kipindi hiki ambacho zimebaki siku chache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.
Amesema kuwa,amani ndiyo ajenda kuu kwa sasa, na hakuna jambo muhimu zaidi kwa Taifa kuliko kudumisha hali hiyo.
Pia, amewakumbusha viongozi wa dini, wanasiasa na waandishi wa habari, ambao ni miongoni mwa makundi yenye ushawishi mkubwa katika jamii, kuhakikisha wanahubiri amani na umoja wakati wote.
Rais Dkt. Mwinyi amepongeza kuanzishwa kwa Jumuiya ya Walimu wa Madrasa, akieleza kuwa ni hatua muhimu inayowaleta pamoja walimu wa Qur’an chini ya chombo kimoja chenye lengo la kudumisha umoja na kuimarisha malezi bora ya Kiislamu kwa watoto na vijana.
Aidha, ameeleza kuwa jumuiya hiyo ni nguzo ya maadili mema na malezi bora, inayowajenga watoto na vijana kuwa raia wema na wachapa kazi kwa manufaa ya Taifa.
Halikadhalika, Dkt. Mwinyi ameshauri kuandaliwa kwa mitaala maalumu ya kufundishia elimu ya dini, ili kuhakikisha watoto wanapata elimu bora yenye mwongozo wa kufundisha unaofanana katika taasisi zote za dini nchini.
Rais Dkt.Mwinyi amehitimisha hotuba yake kwa kusisitiza umuhimu wa kuangalia maslahi ya walimu wa madrasa, kutokana na mchango wao mkubwa katika kuwaelimisha watoto na malezi ya kiroho kwa jamii.Ameahidi katika awamu ijayo ya uongozi wake, atahakikisha walimu hao wanathaminiwa ipasavyo kwa kazi yao ya kujitolea.











