Riba ya Benki Kuu (CBR) yasalia asilimia 5.75 katika robo ya nne,2025

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) inasalia asilimia 5.75 katika robo ya nne ya mwaka inayoanza Oktoba hadi Desemba,2025.
Kiwango cha Riba cha Benki Kuu (CBR) huwa kinatumika na BoT katika shughuli zake na benki za biashara, ambazo zinapaswa kufuata sera hiyo ndani ya wigo uliowekwa na Benki Kuu.

Gavana wa BoT ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha, Bw. Emmanuel Tutuba ameyasema hayo leo Oktoba 2,2025 katika makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam wakati akizungumza katika mkutano na viongozi wa benki na waandishi wa habari.

Amesema, uamuzi huu unatokana na mwenendo mzuri wa kuimarika kwa shughuli za kiuchumi na udhibiti wa mfumuko wa bei nchini, ambapo kamati hiyo ilikutana Oktoba 1,2025.

Hatua hii, pia ni kiashiria kimojawapo katika upangaji wa riba zinazotozwa na mabenki na taasisi nyingine za fedha nchini.

Gavana Tutuba amesema, uamuzi huu unatokana na makadirio ya Benki Kuu ambayo yanaonesha kuwa, uchumi utaendelea kukua na mfumuko wa bei utabaki ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.

Pia,amesema uamuzi wa kutokubadili riba hiyo umetokana na tathmini iliyofanyika kuhusu mwelekeo wa mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi.

Amesema, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.4 mwezi Agosti, na unatarajiwa kubakia, ndani ya lengo la asilimia 3 hadi 5.

Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amesema, makadirio ya BoT yanaonesha kuwa uchumi utaendelea kukua kwa kasi ya kuridhisha.

Pia,ameongeza kuwa,utekelezaji wa sera ya fedha katika robo ya tatu ya mwaka ulifanikiwa kuhakikisha uwepo wa ukwasi wa kutosha kwenye uchumi ambapo ilipelekea kupungua kwa riba ya mikopo ya siku saba baina ya mabenki.

Amesema, BoT ilitumia nyenzo zake za sera ya fedha hasa mikopo ya muda mfupi kwa mabenki kuongeza ukwasi kwenye uchumi.

"Kufuatia hatua hii, hali ya ukwasi iliimarika na kupelekea kupungua kwa riba ya mikopo ya siku saba baina ya mabenki."

Wakati huo huo, Gavana Tutuba amesema, shughuli za kiuchumi ziliendelea kuimarika ambapo kwa upande wa Tanzania Bara, uchumi ulikua kwa asilimia 5.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, ikilinganishwa na asilimia 5.2 katika kipindi kama hicho mwaka 2024.

Amesema, mwenendo huu ulichangiwa zaidi na shughuli za uchimbaji madini, kilimo, huduma za fedha na bima, ujenzi na shughuli za uzalishaji viwandani.

Kwa upande wa Zanzibar, ameeleza kuwa uchumi ulikua kwa asilimia 6.4 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025, sawa na ukuaji uliorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2024 ambapo ukuaji huo ulichangiwa zaidi na shughuli za utalii, ujenzi na kilimo.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ilianza kutekeleza mfumo huu Januari,2024 badala ya mfumo uliokuwa unatumia ujazi wa fedha.

Kupitia mfumo huu, Benki Kuu ya Tanzania huwa inatoa mwelekeo wa riba itakayotumika katika soko la fedha baina ya mabenki.

Lengo la Riba ya Benki Kuu ni kuwezesha ukwasi katika uchumi ili uendane na malengo ya kudhibiti mfumuko wa bei na kuwezesha ukuaji wa uchumi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news