Salamu za Jumapili:Nakupenda sana Mungu

NA LWAGA MWAMBANDE

REJEA neno la Mungu katika Biblia Takatifu kitabu cha Yeremia 29:11 neno la Mungu linasema..."Maana najua mawazo ninayowawazia, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho."
Ukitafakari neno hilo la Mungu utabaini kuwa, hata tunapopitia au unapopitia giza au hali ngumu, Mungu ana mpango mwema.

Hivyo, matumaini yanatufanya tusimame imara tukijua kuwa kesho ni bora kuliko leo.

Kwani, upendo wetu kwa Mungu hauanzishwi na juhudi zetu wenyewe, bali ni jibu kwa upendo wa Mungu ulio wa kweli, wa milele, na usio na masharti.(1Yohana 4:19).

Mungu, yeye alitupenda hata kabla hatujamjua, hata kabla hatujabadilika. Huu ni upendo wa neema unaotuita, kutubadilisha, na kutupa utambulisho wa kweli kama wana wa Mungu.

Huu ndio upendo unaovunja hofu, unaosamehe makosa na unaotuimarisha hata katika udhaifu wetu.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa,Mungu hakutuwekea masharti ili kutupenda na hakuangalia makosa yetu kwanza au mapungufu yetu,bali alitupenda kwanza.

Pia,alimtuma Mwana wake wa pekee Yesu Kristo, si kwa sababu tulikuwa watakatifu, bali kwa sababu tulihitaji wokovu,hivyo upendo wa Mungu ni wa namna yake kwetu,tuendelee kumpenda zaidi.Endelea.

1. Bwana wewe nuguvu zangu, nakupenda sana Mungu,
Wewe ni jabali langu, ngome tena boma langu,
Bwana ni Mwokozi wangu, na tena amani yangu,
Nitakwita Mungu wangu, wastahili kusifiwa.

2. Nakutaja Mungu wangu, wewe ndiye Mwamba wangu,
Ndiwe kimbilio langu, na tena ni ngao yangu,
Pembe ya wokovu wangu, na pia ni ngome yangu,
Nitakwita Mungu wangu, wastahili kusifiwa.

3. Ulipo Mwokozi wangu, hiyo ni salama yangu,
Wawepo watesi wangu, kudhulumu haki yangu,
Utajitokeza Mungu, na kuwa wokovu wangu,
Nitakwita Mungu wangu, wastahili kusifiwa.

4. Kuwe na vitisho kwangu, kutikisa hali yangu,
Na mashambulizi kwangu, dhidi ya amani yangu,
Upo nami Mungu wangu, wanizingira na wingu,
Nitakwita Mungu wangu, wastahili kusifiwa.

5. Wajao adui zangu, kuitaka roho yangu,
Wapige upofu Mungu, wala wasifike kwangu,
Waliko wafunge pingu, wazidi piga majungu,
Nitakwita Mungu wangu, wastahili kusifiwa.

6. Wafukuze wote Mungu, hawana nafasi kwangu,
Umiliki uwe wangu, wa zile baraka zangu,
Na nikutukuze Mungu, kwa matendo yako kwangu,
Nitakwita Mungu wangu, wastahili kusifiwa.

7. Wewe kutosheka kwangu, tena usalama wangu,
Bwana kila kitu kwangu, tena ni kivuli changu,
Muumba nchi na mbingu, ninakuinua Mungu,
Nitakwita Mungu wangu, wastahili kusifiwa.

8. Unipe nafasi Mungu, katika maisha yangu,
Nikutumikie Mungu, kwa moyo na roho yangu,
Nguvu na akili zangu, utukuke wewe Mungu,
Nitakwita Mungu wangu, wastahili kusifiwa.
(Zaburi 18:1-3, 23:1-6, Yoshua 23:5)

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news