Somalia kuanzisha lugha ya Kiswahili katika shule na vyuo vikuu vya ndani

NA DIRAMAKINI 

RAIS wa Jamhuri ya Shirikisho la Somalia, Hassan Sheikh Mohamud ametangaza mpango wa kuharakisha uanzishaji wa lugha ya Kiswahili katika mtaala wa kitaifa wa shule na vyuo vikuu, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano wa Somalia na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Uamuzi huo unaunga mkono jitihada za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kukuza na kuendeleza Kiswahili kote duniani.Tanzania inajivunia kuwa nchi pekee inayounganishwa na lugha ya Kiswahili kote vijijini na mijini. Pichani ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan akimpokea mgeni wake Rais wa Somalia,Mheshimiwa Hassan Sheikh Mohamud aliyefanya ziara nchini Tanzania hivi karibuni.

Katika hotuba yake kwenye Mkutano wa Pili wa Ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EACON2025) uliofanyika mjini Mogadishu siku ya Jumanne, Rais Mohamud aliwahimiza wasomi na taasisi za elimu nchini kuongoza juhudi za kufundisha na kutumia Kiswahili ili kukuza mshikamano wa kikanda.

“Chuo Kikuu cha Taifa cha Somalia, pamoja na vyuo vyote vya Somalia, vinapaswa kuongoza katika kukuza Kiswahili,lugha ya pamoja ya ukanda wa Afrika Mashariki,”alisema Rais Mohamud.

Kiswahili, ambacho huzungumzwa na zaidi ya watu milioni 200 kote Afrika Mashariki na Kati, tayari ni lugha rasmi ya Umoja wa Afrika na ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Sasa, serikali ya Somalia inapanga kukifanya kuwa lugha ya kufundishia sambamba na Kisomali, Kiarabu na Kiingereza.

Waziri wa Elimu nchini Somalia, Farah Sheikh Abdulkadir, alieleza kuwa serikali inashirikiana na taasisi za kikanda kuandaa mfumo madhubuti wa kuingiza Kiswahili katika elimu ya Somalia.

“Tunalenga kukuza masomo na matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini Somalia. Tunataka Kiswahili kitumike kama lugha ya mawasiliano, biashara na elimu na hata kuchukua nafasi ya Kiingereza katika mkutano wetu ujao,” alisema waziri huyo.

Bodi mpya ya Elimu ya Juu ya Taifa inashirikiana kwa karibu na Jumuiya ya Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki pamoja na mfumo wa jumuiya hiyo ili kutekeleza mpango huo.

Somalia ilijiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2024, na kuwa mwanachama wa nane wa jumuiya hiyo, ikijiunga na Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).(Hiiraan)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news