ABU DHABI-Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE),Mheshimiwa Luteni Jenerali mstaafu Yacoub Hassan Mohamed ameikaribisha rasmi timu ya Taifa ya Tanzania katika Ofisi za Konseli Kuu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyopo Dubai.
Timu ya taifa ya Tanzania iliwasili Dubai alfajiri ya Oktoba 12,2025 kwa ajili ya kujiandaa na pambano la kirafiki na Timu ya Taifa ya Iran,mchezo utakafanyika Oktoba 14,2025.
Mheshimiwa Balozi Yacoub pamoja na mambo mengine amewasisitiza viongozi na wachezaji wa timu hiyo kuzingatia nidhamu ya mchezo na wapambane uwanjani ili watoke na ushindi.
Sambamba na hilo Mheshimiwa Balozi Yacoub, aliipongeza timu ya Taifa kwa kuendelea kuimarika kadri ya siku zinavyoenda na kuutaka uongozi kutumia fursa za kujipima uwezo kwa kushinda kila mechi ili ipande chati katika orodha rasmi ya FIFA.
Kwa upande wake Kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania Hemed Seiman Morocco alimshukuru Mheshimiwa Balozi kwa maandalizi mazuri ya uratibu kuanzia siku ya mapokezi hadi wakati huu na kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono sekta ya michezo hususan mpira wa miguu na timu ya taifa kwa ujumla.
Kocha Morocco alitoa shukrani za kipekee kwa namna maandalizi ya mapokezi yao na mwaliko katika ofisi za Konseli Kuu ulivyoratibiwa na kueleza kuwa wameshasafiri nchi nyingi lakini mapokezi ya Ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu ni ya kipekee na ya hali ya juu kabisa na haikuwahi kutokea kupata ukarimu wa aina hiyo nchi zote walizosafiri awali.
Kocha Morocco ameomba ushirikiano wa namna hiyo uendelee kufanyika katika maeneo yote Timu ya Taifa itaposafiri na kueleza kuwa jambo hilo limeifanya timu hiyo kujisikia ipo katika mikono salama na kupata motisha zaidi ya kupambana na kuhakikisha ushindi unapatikana.Amesema Timu ya Taifa ya Tanzania ipo katika hali nzuri kiafya na kimchezo na kumtaka na kwamba Watanzania wategemee burudani safi siku ya mchezo huo.
Aidha Uongozi wa Timu ya Taifa kupitia Kocha mkuu wa Timu hiyo Ulimkabidhi Mheshimiwa Balozi Jezi ya Timu ya Taifa ya Tanzania ikiwa ni kama kumbukumbu yake.












