NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) leo Oktoba 22,2025 imetoa taarifa kwa wananchi na wadau wote kuhusu hali ya hewa inayoendelea, hususan kuhusiana na kutokea kwa kimbunga chenye nguvu kinachofahamika kwa jina la CHENGE.


Kimbunga hicho kipo katika Bahari ya Hindi, Kaskazini Mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar umbali wa takribani kilomita 2400 kutoka Mashariki mwa pwani ya Mtwara.
Kwa mujibu wa takwimu na uchambuzi wa hali ya hewa wa hivi karibuni, Kimbunga CHENGE kilianza kujitokeza katika maeneo ya Mashariki ya Bahari ya Hindi mnamo Oktoba 17,2025.
Tangu wakati huo, kimbunga hicho kimeendelea kuimarika, kikisalia katika eneo husika huku kikikusanya nguvu zaidi kutokana na hali ya joto ya bahari na mienendo ya anga.
TMA imebainisha kuwa,kwa sasa kimbunga hicho kipo umbali wa takribani kilomita 2,400 kutoka mashariki mwa pwani ya Mtwara, Tanzania.
Uchambuzi wa kitaalamu wa mifumo ya hali ya hewa unaonesha kuwa katika kipindi cha siku nne hadi tano zijazo kati ya tarehe 26 hadi 27 Oktoba, 2025 kimbunga hicho kinatarajiwa kusogea kuelekea Magharibi mwa Bahari ya Hindi, kuelekea ukanda wa pwani ya Tanzania, ingawa kwa wakati huo kinatarajiwa kuwa kimepungua nguvu.
Aidha,kwa mujibu wa taarifa hiyo TMA inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa kimbunga CHENGE pamoja na athari zake zinazoweza kujitokeza katika mifumo ya hali ya hewa ya ndani ya nchi, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuathiri hali ya hewa katika maeneo ya ukanda wa pwani.
Vilevile,mamlaka imewakumbusha watumiaji wa bahari wakiwemo wavuvi, wasafirishaji wa baharini na wadau wengine wa sekta ya uchukuzi.
Sambamba na wananchi kwa ujumla, kuendelea kufuatilia kwa ukaribu taarifa rasmi za hali ya hewa zitakazotolewa na TMA kupitia vyombo vya habari, tovuti rasmi pamoja na majukwaa rasmi ya mitandao ya kijamii ya mamlaka.
Aidha, inashauriwa kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalamu wa kisekta ili kuchukua tahadhari stahiki kwa lengo la kulinda maisha,malina shughuli za kiuchumi.
TMA itaendelea kutoa taarifa za mwelekeo na maendeleo ya kimbunga CHENGE kwa wakati muafaka kadri hali itakavyobadilika.
Vimbunga
Kwa mujibu wa World Meteorological Organization (WMO)- Cyclone Terminology and Tracking (2023),vimbunga ni mojawapo ya matukio hatari ya kijiografia yanayojitokeza mara kwa mara katika maeneo ya kitropiki.
Aidha,ni mifumo mikubwa ya hali ya hewa inayoambatana na upepo mkali, mvua kubwa, na mawimbi ya bahari yanayoweza kusababisha madhara makubwa kwa maisha ya binadamu,mali na mazingira.
Tanzania, ingawa haiko katika ukanda wa vimbunga vya moja kwa moja, kupitia TMA imeendelea kuwa na mifumo imara ya ufuatiliaji na tahadhari, hasa kutokana na uwepo wa Bahari ya Hindi ambayo ni chimbuko kuu la vimbunga.
Tags
CHENGE Cyclone
Habari
Kimbunga
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
Vimbunga