NA DIRAMAKINI
IKIWA imesalia saa zaidi ya 150 Watanzania wamiminike katika vituo vya kupigia kura kote nchini, hapa Zanzibar kwa kauli moja tumeazimia kumrejesha tena Ikulu kwa kishindo, mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi.
Dkt.Mwinyi amefanya mengi na ameendelea kuonesha mfano wa uongozi unaojengwa juu ya misingi ya maadili, haki na hofu ya Mungu.
Tangu achukue hatamu za uongozi wa Zanzibar mnamo Novemba 2020, Dkt. Mwinyi ameweka msisitizo mkubwa kwenye uwazi, uwajibikaji, na kupambana na rushwa ikiwa ni mambo yanayoakisi uongozi wa kumcha Mungu.
Kwa kuzingatia mafunzo ya kidini na maadili ya kijamii, Dkt.Mwinyi amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kuwa viongozi na watendaji wa serikali wanatumikia wananchi kwa uaminifu na uadilifu.
Aidha,katika hotuba zake mbalimbali, mara kwa mara amesisitiza umuhimu wa kutenda haki kwa wote, bila kujali hadhi au nafasi ya mtu katika jamii.
Kauli hizi zimeambatana na vitendo vya wazi, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua dhidi ya viongozi waliobainika kutumia madaraka vibaya au kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Moja ya mafanikio makubwa chini ya uongozi wake ni kuimarika kwa hali ya utulivu, mshikamano wa kitaifa na ushirikiano kati ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano.
Pia, amesisitiza juu ya amani na maridhiano ya kisiasa,mambo ambayo ni msingi wa maendeleo ya kweli na ustawi wa wananchi.
Dkt.Mwinyi ni kiongozi anayeheshimu thamani ya maisha ya kila mtu na mara kwa mara ameonesha huruma na kujali maslahi ya wananchi, hasa wanyonge.
Ukaribu wake na watu wa kawaida, pamoja na kujitahidi kutatua changamoto zao kwa njia ya amani na haki ni ishara wazi ya moyo wa kumcha Mungu.
Kwa ujumla, uongozi wa Dkt.Hussein Ali Mwinyi umeonesha kuwa siasa ni maendeleo na inaweza kuwa njia ya kutumikia watu kwa moyo wa uadilifu na kwa kumtegemea Mungu.
Ni dhahiri kuwa maono yake yanatafsiriwa kwa vitendo vinavyolenga kuijenga Zanzibar mpya, yenye maendeleo, usawa na heshima kwa kila raia.
Kwa muktadha huu,tuandae na kuziweka kadi zetu za kupigia kura mahali salama ili Oktoba 29 ikifika, mapema asubuhi tunamaliza kazi ya kumrejesha Ikulu kwa kishindo Dkt.Mwinyi, kiongozi wa watu,mwenye hofu ya Mungu na msimamizi wa maendeleo ya kweli.









