NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa Kimbunga CHENGE kilichopo katika Bahari ya Hindi, kaskazini mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar ambacho kwa sasa kimeanza kusogea kuelekea magharibi mwa upande wa pwani ya Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA,hadi kufikia asubuhi ya leo Oktoba 24,2025, Kimbunga CHENGE kilikuwa kimepiga kambi umbali wa takribani kilomita 1,680 mashariki mwa pwani ya Mtwara, kikisababisha mabadiliko ya mifumo ya hali ya hewa katika eneo lote la Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Pia, kwa mujibu wa uchambuzi wa wataalamu wa TMA, kimbunga hicho kinatarajiwa kuendelea kusogea kuelekea Magharibi huku nguvu yake ikipungua taratibu kadri kinavyokaribia ukanda wa pwani.
Hali hii inaweza kusababisha vipindi vya mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa baharini kati ya tarehe 26 hadi 28 Oktoba,2025, hususan katika mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Dar es Salaam na Tanga, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
TMA imesisitiza kuwa, kwa sasa, athari kubwa hazitarajiwi, lakini wananchi wanapaswa kuwa makini na kufuatilia taarifa rasmi zitakazotolewa kila mara.
Mamlaka hiyo imebainisha kuwa, inaendelea kufuatilia mwenendo wa Kimbunga CHENGE saa 24 kwa siku na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati.
Katika hatua nyingine, TMA imewataka watumiaji wa bahari wakiwemo wavuvi na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa kupitia vyombo rasmi vya mamlaka hiyo na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.
Tags
CHENGE Cyclone
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
