Tumefuta chuki na ubaguzi,tumejenga Zanzibar inayowakumbatia wote-Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuondoa ubaguzi, mifarakano na siasa za chuki katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Akizungumza katika mkutano na viongozi wa dini, masheikh, watawa na mapadri uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Skuli ya Utaani, Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, leo tarehe 05 Oktoba 2025, Dkt. Mwinyi amesema kuwa umoja wa Wazanzibari ndio nguzo kuu ya mafanikio ya Serikali na maendeleo ya Taifa.

Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane chini ya CCM imefanikiwa kuimarisha maridhiano, umoja wa kitaifa na kuondoa ubaguzi katika nafasi na majukumu ya kitaifa, kwa maslahi ya wananchi wote.
Rais Dkt. Mwinyi amesema mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta za elimu, afya, ustawi wa jamii, huduma za maji na miundombinu, akisisitiza kuwa Serikali tayari imeifungua Pemba kimaendeleo na kiuchumi.

Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara, bandari na viwanja vya ndege ni nyenzo muhimu za kuifungua nchi kiuchumi, ambazo Serikali itaendelea kuimarisha katika awamu ijayo.

Aidha, Dkt. Mwinyi amewahakikishia viongozi wa dini na wananchi kuwa Serikali itaendelea kuyashirikisha madhehebu na dini zote bila ubaguzi katika kujadili masuala ya kitaifa na ustawi wa jamii.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Muhammed Said Dimwa, amemuelezea Dkt. Mwinyi kuwa ni kiongozi muadilifu, mpenda amani na maendeleo, na kuwataka wananchi wa Pemba kumpa ridhaa tena ili aendelee kuleta maendeleo zaidi.

Naye, Katibu Mtendaji wa Afisi ya Mufti wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume, amesema ajenda kuu za dini ni uadilifu, haki, mshikamano na amani, ambazo kila mmoja anapaswa kuzizingatia kwa manufaa ya jamii na Taifa.
Rais Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa maovu yanayoendelea ndani ya jamii yanahitaji ushirikiano wa Serikali na taasisi za dini na kijamii kuyadhibiti, akisema si jukumu la Serikali pekee.

Amewaomba wananchi wa Pemba kumuamini kwa awamu nyingine na kumpa nafasi ya kuendelea kuiongoza Zanzibar kwa mafanikio na maendeleo zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news