NA DIRAMAKINI
KLABU ya Yanga SC (Young Africans Sports Club) imetangaza kuondoa viingilio katika mchezo wake wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAF Champions League) dhidi ya Silver Strikers ya Malawi.
Mtanange huo utapigwa Oktoba 25, 2025 kwenye dimba la Benjamin Mkapa lililopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 21,2025 na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ali Shaban Kamwe katika mkutano na waandishi wa habari uliolenga kueleza maandalizi ya mchezo huo wa kihistoria.
“Tumepokea maombi mengi kutoka kwa Wanachama wetu waliotaka mechi hii isiwe na viingilio,baada ya majadiliano,uongozi umeafiki na kuidhinisha ombi hilo.Hili ni pambano la Wananchi,tuwaachie wao na waibebe timu yao."
Kwa mujibu wa Kamwe, viingilio vimeondolewa katika majukwaa yote isipokuwa VIP A na VIP B, ambayo yatabaki kuwa maalum kwa wageni waalikwa na wanachama wa Yanga waliopo kwenye mpango wa ‘Black Card’.
Hatua hii imeelezwa kuwa,ni ishara ya kuthamini mchango na mapenzi ya mashabiki, huku uongozi wa klabu ukitambua changamoto za kifedha zinazolikabili benchi la ufundi na uendeshaji wa timu.
“Haikuwa uamuzi mwepesi. Tuna mahitaji mengi ya kuiendesha timu. Lakini kwa umuhimu wa mchezo huu,tumeamua kuweka mbele maslahi ya ushindi,”ameongeza Kamwe.
Katika kuelekea mchezo huo wa kusaka tiketi ya hatua ya makundi, Kamwe ameeleza kuwa, kikosi cha Yanga tayari kipo kambini tangu leo saa 6 mchana, huku mshambuliaji Clement Mzize akithibitishwa kuwa fiti kiafya.
“Mzize yupo fiti kabisa.Kama itampendeza mwalimu, basi atakuwa sehemu ya kikosi siku ya mechi.”
Kwa upande wa benchi la ufundi, Yanga itashuka dimbani chini ya kocha wa muda (caretaker coach),Patrick Mabedi huku mchakato wa kumpata kocha mpya ukiwa mbioni kukamilika ndani ya siku tatu zijazo.
“Hatuna wasiwasi na Mabedi. Tunaamini katika uwezo wake na uzoefu wake katika soka la Afrika.”
Kamwe pia amebainisha kuwa, wapinzani wao, Silver Strikers, wanatarajiwa kuwasili nchini Alhamisi saa 2 usiku, na watafanya mazoezi siku moja kabla ya mechi, huku muda rasmi wa mazoezi yao ukitarajiwa kutangazwa kwa vyombo vya habari.
Pia,Kamwe amesisitiza kuwa,mechi hiyo ni ya Wananchi wa Yanga, akionya vikali wale wenye nia tofauti na mchezo wa soka.
“Mageti yatafunguliwa kuanzia saa 2 asubuhi. Kama si Mwanayanga na unakuja na dhamira ovu, tutalaumiana. Usije na ajenda nyingine. Tunawaalika watu wanaopenda mpira kwa dhati,vinginevyo, kaa mbali,”amesisitiza Kamwe
Aidha,mechi hiyo inatarajiwa kuvuta maelfu ya mashabiki,si tu kwa sababu ya umuhimu wake kisoka,bali pia kutokana na uamuzi wa kihistoria wa kuifanya bure kwa mashabiki wote.
