Umoja,Amani na Mshikamano ndizo nguzo za Taifa letu jitokezeni kupiga kura-Rais Dkt.Mwinyi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amewahakikishia wananchi kuwa kutakuwa na ulinzi wa kutosha siku ya uchaguzi, na amewataka wajitokeze kwa wingi kutimiza haki yao ya kidemokrasia kwa amani na utulivu.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo Oktoba 25,2025 alipohudhuria Maombi ya Amani ya Kitaifa yaliyoandaliwa na Jumuiya ya Wakristo Zanzibar yaliyofanyika katika Uwanja wa Kizimbani Dole uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema kuwa, Serikali zote mbili zimejiandaa kikamilifu kuhakikisha kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura anapata fursa ya kutekeleza haki yake ya kikatiba ya kuchagua viongozi anaowataka.
Ameongeza kuwa amani, muungano na mshikamano ni nguzo kuu za taifa ambazo CCM imeziahidi kuzilinda kwa maslahi ya wananchi wote, bila kujali asili au dini zao.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kuwa Serikali imeondoa aina zote za ubaguzi, ikiwemo ubaguzi wa dini, na itaendelea kudumisha sera ya kutoa uhuru wa kuabudu kwa waumini wa imani zote.

Amewashukuru viongozi wa Umoja wa Makanisa kwa kuandaa maombi hayo, akisema yana umuhimu mkubwa hasa katika kipindi hiki cha kampeni na kuelekea uchaguzi mkuu.

Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza wajibu wa taasisi za kidini katika kuwaandaa waumini kuwa raia wema na kuchangia maendeleo ya nchi, huku akiahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nazo katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi.

Vilevile Dkt.Mwinyi ameahidi kuendeleza ushirikiano na Umoja wa Makanisa katika awamu ijayo, endapo wananchi watakipa ridhaa CCM kuendelea kuiongoza Zanzibar, huku akizipongeza taasisi hizo kwa mchango wao katika sekta za elimu, afya na maji.
Kwa upande wake, Askofu Dickson Kaganga, Mwenyekiti na Mratibu wa maombi hayo, ameahidi kwa niaba ya Umoja wa Makanisa Zanzibar kuendelea kuiombea nchi amani, umoja na mshikamano, na kuwasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa utulivu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news