ZANZIBAR-Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi ameonesha mshikamano na kuthamini juhudi za wananchi kwa kutembelea soko la mazao ya baharini katika Kijiji cha Kikungwi kilichopo Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, akiwa ameambatana na mke wake, Mama Mariam Mwinyi.
Ziara hiyo ya ghafla Oktoba 16,2025 ilifanyika baada ya mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika katika eneo la Paje, ambapo Dkt. Mwinyi alipata fursa ya kuzungumza na wajasiriamali wa eneo hilo wanaojishughulisha na biashara ya chaza.
Hili ni zao muhimu la baharini linaloendelea kuchangia katika pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
“Tulifurahia kuzungumza na wajasiriamali wa eneo hili ambao kwa juhudi na bidii zao wanachangia katika uchumi wa kaya na maendeleo ya taifa letu kupitia biashara ya mazao ya baharini,"amesema Dkt.Mwinyi.
Aidha, ameeleza kuwa,sekta ya uchumi wa buluu ina nafasi ya kipekee katika kufanikisha maendeleo endelevu ya Zanzibar, na akasisitiza dhamira yake ya kuimarisha uzalishaji wa mazao ya baharini kwa njia bora, salama na endelevu.“Ninazidi kuthamini kazi kubwa inayofanywa na wananchi wetu katika sekta hii muhimu ya uchumi wa buluu. Tuweke mkazo zaidi katika kuendeleza shughuli za uzalishaji wa mazao ya baharini kwa njia endelevu, ili manufaa yake yawafikie Wazanzibari wote,"ameongeza.
Aidha,ziara hiyo imepokelewa kwa furaha kubwa na wananchi wa Kikungwi, ambao wameeleza kuwa kuguswa moja kwa moja na kiongozi wa juu ni ishara ya uongozi wa karibu na unaojali maisha ya watu wa kawaida.
