ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameungana na waumini wa dini ya Kiislamu katika Sala ya Ijumaa iliyoambatana na dua maalum ya kuombea amani ya nchi pamoja na uchaguzi mkuu ujao.
Ibada hiyo imefanyika leo Oktoba 17,2025 katika Msikiti wa Muembe Shauri uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali,viongozi wa dini, pamoja na wananchi kutoka maeneo tofauti ya mkoa huo.
Katika hotuba yake kwa waumini na wananchi waliohudhuria ibada hiyo, Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kudumisha amani na utulivu kama msingi wa maendeleo ya taifa.
“Kudumisha amani ni jukumu la kila mmoja wetu. Amani ni nguzo kuu ya umoja na maendeleo katika nyanja zote za maisha, hivyo ni wajibu wetu kuilinda kwa maneno na matendo mema,"Rais Dkt.Mwinyi amewakumbusha wananchi.
Amesema kuwa,maendeleo makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne iliyopita yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuwepo kwa hali ya amani na utulivu, hali ambayo imesaidia Serikali kutekeleza mipango na miradi yake kwa ufanisi.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi ameonya kuwa vurugu au migogoro ya kisiasa haianzi kwa silaha, bali mara nyingi huanza kwa maneno na matendo madogo ambayo huweza kuchochea hali ya sintofahamu.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amesisitiza umuhimu wa kuchunga kauli na kuendeleza mazungumzo ya kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.“Tuchunge kauli zetu, tuendelee kuhubiri amani, na tuilinde nchi yetu. Amani ni msingi wa maendeleo-tuihifadhi, tuiheshimu, tuiishi,” ameongeza.
Rais Dkt.Mwinyi pia amewahimiza wananchi wote kudumisha utulivu kabla, wakati na baada ya uchaguzi, huku akisisitiza utii kwa sheria na taratibu zitakazotolewa na Tume ya Uchaguzi katika kipindi chote cha uchaguzi.
Kauli ya Rais Dkt.Mwinyi imekuja wakati taifa likijiandaa kwa uchaguzi mkuu, ambapo kampeni za kisiasa zipo katika kipindi cha lala salama visiwani Zanzibar na Tanzania Bara kwa ujumla.


















