Vinne makundi CAF


KATIKA msimu wa 2025/26 wa mashindano ya Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), klabu nne za Tanzania zimefanya vizuri kwa kufanikiwa kufika hatua ya makundi.
Simba Sports Club (Simba SC) na Young Africans Sports Club (Yanga SC) zimeshinda nafasi zao kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAF Champions League).

Aidha, Azam FC na Singida Black Stars wameingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF Confederation Cup) kwa mara ya kwanza.

Ushiriki huu si tu unaongeza heshima ya klabu na taifa kwenye soka la Afrika, bali pia unaleta faida za kifedha kupitia zawadi za CAF, matangazo na viingilio vya mechi.

Vilevile, wachezaji wanapata uzoefu wa kimataifa unaosaidia kuboresha kiwango cha timu.

Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema, kwa jumla, mafanikio haya yanaonesha maendeleo makubwa ya soka la Tanzania barani Afrika na kutoa fursa kwa klabu kuongeza umaarufu, mapato na kuimarisha kiwango cha wachezaji. Endelea;

1. Ni pongezi Tanzania, hili soka la Afrika,
Vinne vimeingia, makundi kwa uhakika,
Ubora unachangia, ligi imechangamka,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

2. Katika klabu bingwa, hapa barani Afrika,
Tuna timu mbili bingwa, mtoano zimevuka,
Timu ngeni zimegongwa, msimamo zikashuka,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

3. Hapa ni Yanga na Simba, makundi CAF Afrika,
Nchi yetu tunatamba, tunapoitaja soka,
Na TFF vimba, vema mnawajibika,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

4. Michuano Shirikisho, hapa barani Afrika,
Huko nako si wa mwisho, timu mbili zimevuka,
Sasa ni matayarisho, mbele zaidi kufika,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

5. Azam walishtua, timu livyoitandika,
Ilikuwa ni butua, magoli tisa hakika,
Lengo lao wanajua, kule wataka kufika,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

6. Kisha Singida wenzetu, nao wamechakarika,
Wamefanya vyao vitu, makundi watatajika,
Hili jambo kubwa kwetu, makundi tuvyoyashika,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

7. Wakati Simba na Yanga, makundi wazoeleka,
Wengine wanajipanga, mara ya kwanza kufika,
Ni kibabe wametinga, nchi itanufaika,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

8. Hongera TFF, jinsi mnawajibika,
Timu kuzipiga tafu, ziweze kuchangamka,
Hata sasa twazisifu, pira letu lainuka,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

9. Pia Serikali yetu, hapa nayo yahusika,
Hamasa kwa timu zetu, kwa kweli inasikika,
Sifa kwa taifa letu, hiyo inaongezeka,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

10. Heri tunazitakia, zizidi kuchakarika,
Mbali ziweze fikia, wapinzani kiwafyeka,
Pesa zizidi ingia, nchi ikineemeka,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

11. Hata wachezaji wetu, cheza mzidi uzika,
Muwe ni Samata wetu, huko nje kutumika,
Iwe ni faida kwetu, ujuzi kuongezeka,
Vinne makundi CAF, hii ni hatua kubwa.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news