Watumishi wa umma Oktoba 29 mkatimize haki yenu ya Kikatiba-Msajili wa Hazina

NA GODFREY NNKO

OFISI ya Msajili wa Hazina (OMH) imewakumbusha na kuwasisitiza watumishi wote wa umma waliopo katika taasisi na mashirika ya umma kote nchini kutumia haki yao ya msingi ya kikatiba kwa kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29,2025.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 27,2025 na Mkurugenzi wa Usimamizi wa Utendaji, Ufuatiliaji na Tathmini - Mashirika ya Kibiashara, Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bi. Lightness Mauki wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kwa niaba ya Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu.

Amesema,Ofisi ya Msajili wa Hazina ambayo imeanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Msajili wa Hazina (Madaraka na Majukumu), Sura ya 370, ina jukumu la kusimamia na kuendeleza uwekezaji wa Serikali katika taasisi na mashirika ya umma na kampuni ambazo Serikali ina hisa au maslahi.

"Pamoja na majukumu hayo, Ofisi pia inahakikisha usimamizi bora na ustawi wa rasilimaliwatu waliopo katika taasisi hizo ili kuimarisha uwajibikaji, uadilifu, na mchango wao kwa maendeleo ya Taifa.

"Katika kuzingatia majukumu hayo, Ofisi inawakumbusha watumishi wote katika taasisi na mashirika ya umma kwamba kushiriki uchaguzi ni wajibu wa kiraia unaojenga demokrasia, umoja na uthabiti wa Taifa."

Msajili wa Hazina amesisitiza kuwa,kupiga kura ni chombo cha mabadiliko chanya, kinachowawezesha wananchi kuchagua viongozi wenye maono, uadilifu, na uwajibikaji.
"Hivyo,ushiriki mkubwa wa watumishi wa umma unaonesha mfano wa uzalendo, nidhamu ya kitaifa na uelewa wa majukumu ya kikatiba.

"Ofisi ya Msajili wa Hazina inaamini kuwa, kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi huu, watumishi wa umma wataendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha utawala bora, uchumi endelevu na ustawi wa wananchi.

"Kwa mantiki hiyo, Ofisi inatoa wito kwa wakuu wa taasisi na mashirika ya umma kuhakikisha kwamba watumishi wao wanapatiwa fursa ya kutekeleza haki hii muhimu bila kuathiri majukumu yao ya kikazi, kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi,"amesisitiza Msajili wa Hazina.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news