NA DIRAMAKINI
KLABU ya Yanga SC (Young Africans Sports Club) ya jijini Dar es Salaam imeiondosha Silver Strikers FC ya Malawi nje ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CAFCL) kwa kuichapa mabao 2-1.
Ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya marudiano Oktoba 25,2025 ndani ya dimba la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam umeiwezesha Yanga SC kutinga hatua ya makundi ya CAFCL kwa mara ya tatu mfululizo.Shukrani kwa Dickson Job ambaye alipachika bao la kwanza dakika ya 5' na Pacome Zouzoua aliyezamisha jahazi kwa bao la pili dakika ya 33', ambalo lilifunga mahesabu.
Singida Black Stars yaichapa Flambeau du Centre mabao 4-2
Mbali na hayo,Singida Black Stars imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAFCC) kwa mara ya kwanza katika historia kufuatia ushindi wa jumla wa mabao 4-2 dhidi ya Flambeau du Centre ya Burundi kwenye hatua ya pili.
Singida Black Stars imevuna ushindi huo katika dimba la Azam Complex lililopo Kata ya Chamanzi Halmashauri ya Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam.
Malanga Horso Mwaku ndiye aliyeanza kurejesha matumaini ya Singida Black Stars kusonga mbele baada ya dakika ya 55 ya kipindi cha pili kupachika bao la kwanza, dakika ya 67, Clatous Chama alirejea nyavuni kwa kuongeza bao la pili, huku Idrissa Diomande dakika ya 72 akifunga bao la tatu.
Ushindi huo ulivuruga misheni ya Flambeau du Centre ambayo tayari ilikuwa na bao la mapema lililofungwa dakika ya 26 na David Irishura.
Mechi ya awali ilipigwa katika uwanja wa Stade Intwari nchini Burundi ambapo Singida Black Stars na Flambeau du Centre ziliibuka na matokeo ya bao 1-1.
Katika mtanage huo,Singida Black Stars ilionesha njia baada ya Clatous Chama kufunga bao dakika ya 60, ingawa bao hilo halikudumu, kwani Flambeau du Centre walijibu mapigo dakika ya 62 kupitia Edson Munaba.
Azam FC yatinga hatua ya makundi
Oktoba 24,2025 historia iliandikwa kwa Azam FC kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAFCC) kwa mara ya kwanza.
Ni baada ya ushindi wa jumla ya mabao 9-0 dhidi ya KMKM FC kwenye hatua ya pili ya CAFCC.
Azam FC ilishinda mabao 2-0 kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza kabla ya kushinda mabao 7-0 kwenye marudiano katika dimba la Azam Complex, Chamazi jijini Dar es Salaam.
Mabao hayo yalifungwa na Idd Nado dakika ya 23, Jephté Kitambala dakika ya 27, Kitambala tena dakika ya 30, Nando tena dakika ya 43, Pascal Msindo dakika ya 49 huku Abdul Sopu akifunga mabao mawili dakika ya 53 na 57 ya mchezo huo.
Tags
AZAM FC
Habari
KMKM
Kombe la Klabu Bingwa barani Afrika
Kombe la Shirikisho Afrika
Michezo
Silver Strikers FC
Singida Black Stars
Yanga SC
Young Africans Sports Club


