ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi leo Oktoba 27,2025 ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo jipya la huduma za akina mama na watoto katika Hospitali ya Makunduchi iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada endelevu za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) za kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Dkt.Mwinyi amesema,dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kila Mzanzibari anapata huduma za afya bora,salama na zenye ubora katika kila ngazi ya utoaji huduma.
Pia,amebainisha kuwa, Serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi na ukarabati wa hospitali za wilaya na mikoa, ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mnazi Mmoja na Hospitali ya Saratani Binguni kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha mfumo wa afya nchini.“Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila ubaguzi, na kwa wakati, kwa sababu afya njema ndiyo msingi wa maendeleo ya jamii,” alisema Dkt. Mwinyi.
Mradi wa ujenzi wa jengo hilo jipya la huduma za akina mama na watoto una thamani ya shilingi bilioni 2.5 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi tisa hadi mwaka mmoja.
Utekelezaji wa mradi huu unaofanywa na Kampuni ya Quality Building Constructor utawanufaisha zaidi ya wananchi 9,800 kutoka shehia 21 za Wilaya ya Kusini ambapo Raia Dkt.Mwinyi amemtaka mkandarasi kufanya kazi kwa bidii na kuzingatia ubora.
Aidha,huduma zitakazotolewa ni pamoja na huduma za uzazi salama, ultrasound, huduma za watoto wachanga na huduma za maabara.Dkt. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuwashukuru wafadhili na wadau wa maendeleo waliounga mkono mradi huo, akiwemo Taasisi ya Fumba Port, Lady Fatuma Foundation na Jaffer Foundation, kwa mchango wao mkubwa wa kifedha na moyo wa kujitolea katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha sekta ya afya.
“Serikali inatambua kwamba haiwezi kutekeleza kila jambo peke yake, hivyo ushirikiano wa wadau wa maendeleo ni muhimu sana katika kuokoa maisha na kuinua ustawi wa jamii yetu,”amesisitiza Rais Mwinyi.
Vilevile,kupitia mradi huu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwekeza katika afya ya mama na mtoto kama nguzo muhimu ya maendeleo endelevu, huku ikihakikisha huduma bora, zenye ubora wa kimataifa, zinapatikana hadi ngazi za vijiji.

















