MWANZA-Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya kijamii ili kuimarisha usalama na kudhibiti uhalifu, ambapo limekutana na maafisa usafirishaji wa Kanda ya Igoma, Wilaya ya Nyamagana.
Akizungumza katika mkutano huo, Novemba 29 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, ameeleza kufurahishwa na ushiriki wa kundi hilo, huku akisisitiza umuhimu wa kuzingatia elimu ya usalama barabarani waliyopewa.
Amesema ongezeko la ajali za barabarani linatokana na uzembe wa baadhi ya waendesha vyombo vya moto hivyo akataka kila mmoja kuwajibika ipasavyo kukomesha ajali hizo.
Amesisitiza kuwa,utii wa sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani ni wajibu wa kila mtumiaji wa barabara huku akiwaonya dhidi ya makosa hatarishi kama vile kuendesha bila kofia ngumu, kupuuza taa za barabarani, kubeba abiria zaidi ya mmoja, kuendesha bila leseni au mafunzo rasmi ya udereva.
Aidha, amewakumbusha wananchi wa Mkoa wa Mwanza kuepuka kujihusisha na vurugu kama zilizotokea tarehe 29 Oktoba 2025, akisisitiza kuwa matatizo yoyote ya kisheria yashughulikiwe kwa kufuata taratibu badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Amewasihi waendesha bodaboda kuwa mabalozi wa amani na usalama kwa kutoshiriki au kushawishiwa kushiriki vitendo vya uchochezi au uharibifu wa mali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, SSP Ibrahim Sunday, amewataka maafisa usafirishaji kuhakikisha wanakuwa na bima halali, leseni ya udereva na kufuata sheria zote za usalama barabarani.
Naye, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, SSP Virginia Sodoka, amewataka waendeleze mshikamano na kushirikiana kwa karibu na vyombo vya usalama kwa kutoa taarifa za uhalifu au vitendo vyovyote vinavyohatarisha usalama kwenye sekta ya usafirishaji ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa usafirishaji wa Kanda ya Igoma, Katibu wa Umoja wa Waendesha Pikipiki Mkoa wa Mwanza, Kudra Salum, ameahidi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za kihalifu na kuchukua hatua dhidi ya wanachama wanaokiuka sheria na kujihusisha na vitendo vya uhalifu.




