BoT ilivyosimama imara kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa na uchumi imara,shindani na endelevu

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) inaendelea kuwa nguzo muhimu katika ustahimilivu na ukuaji wa uchumi wa nchi, huku ikiimarisha utekelezaji wa sera za kifedha zinazolenga kudhibiti mfumuko wa bei na kuimarisha uthabiti wa mfumo wa kifedha nchini.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 19,2025 jijini Dodoma na Meneja Msaidizi wa Uchumi kutoka BoT tawi la Dodoma, Shamy Chamicha wakati akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya Benki Kuu, na maana ya Sera ya Fedha inayotumia Riba ya Benki Kuu katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara nchini.

Semina hiyo inayoratibiwa na BoT inawajumuisha waandishi wa habari kutoka Dodoma, Pwani, Dar es Salaam, Morogoro na Zanzibar.

Bw.Chamicha amesema, jukumu la msingi la BoT ni kuandaa na kutekeleza sera ya fedha inayolenga kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki katika viwango vinavyokubalika na kuendelea kujenga mazingira yenye uthabiti unaochochea ukuaji endelevu wa uchumi wa nchi.

Katika kutekeleza dhamana hiyo, amesema BoT hutumia nyenzo mbalimbali za sera za fedha kama vile udhibiti wa ukwasi, usimamizi wa viwango vya riba, na ufuatiliaji wa mwenendo wa masoko ya fedha ili kuhakikisha uchumi unakuwa katika mkondo salama na thabiti.

Amesema,hatua hizo zimekuwa muhimu katika kukabiliana na misukosuko ya kiuchumi ndani na nje ya nchi, ikiwemo mabadiliko ya bei za bidhaa duniani na shinikizo la mahitaji ya fedha katika soko la ndani.
Mbali na jukumu hilo kuu, amesema Benki Kuu ya Tanzania ina majukumu mengine muhimu yanayosaidia kuimarisha sekta ya fedha na ustahimilivu wa uchumi ikiwemo kutoa sarafu ya nchi, ambayo ni Shilingi ya Tanzania, na kuhakikisha usalama, ubora na upatikanaji wake katika mzunguko kote nchini.

Pia, amesema BoT inasimamia na kudhibiti mabenki na taasisi za fedha, kwa lengo la kuhakikisha zinatoa huduma salama, kwa ufanisi na kwa kufuata misingi ya kisheria na kitaasisi ili wananchi waweze kunufaika na huduma zao.

Jukumu lingine amesema, ni kusimamia mifumo ya malipo nchini, ikiwemo kuhakikisha miamala ya kifedha inafanyika kwa usalama, kwa wakati na kwa gharama nafuu kote nchini.

Bw.Chamicha amesema, jukumu lingine ni kuhifadhi akiba ya nchi, ikijumuisha fedha za kigeni ili kusaidia uthabiti wa shilingi na uwezo wa nchi kukabiliana na changamoto za kiuchumi zinazoathiri mizania ya malipo.
Vilevile, BoT inatimiza jukumu lake kama Benki ya Serikali, ikiwemo kusimamia akaunti za serikali na utekelezaji wa shughuli za kifedha kwa niaba ya serikali.

"Pia, Benki Kuu ni benki ya mabenki, inahakikisha mabenki mengine yanapata huduma za msingi za kifedha,ikiwa ni pamoja na usimamizi wa ukwasi na huduma za malipo nchini."

Aidha, amesema, BoT huwa inatoa ushauri kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhusu masuala ya uchumi na fedha, hususan yanayohusiana na sera za fedha,masoko ya fedha na mwenendo wa uchumi wa ndani na kimataifa.

Katika hatua nyingine, Bw.Chamicha amesema, Sera ya Fedha inayotumia Riba ya Benki Kuu imeendelea kuleta matokeo chanya nchini tangu ianze kutekelezwa rasmi mapema mwaka 2024.
“Kupitia sera za fedha, benki hufanya tathmini ya mara kwa mara kuhusu mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki kudhibiti ongezeko au upungufu wa fedha kwenye mzunguko. Kabla ya sera hii, uchumi wa Tanzania ulikabiliwa na changamoto za riba kubwa na bei zisizo thabiti. Lakini sasa tunayo uthabiti zaidi katika fedha zetu, na uchumi unaonesha ukuaji thabiti."

Sera ya fedha inajumuisha hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania ili kubadili ujazi wa fedha na viwango vya riba.

Hii hufanywa kwa kutumia nyezo za sera ya fedha ambazo Benki Kuu huona kuwa zinafaa kutumika kwa kipindi husika.

Katika kutimiza jukumu hili, Benki Kuu hufanya tathimini ya hali ya uchumi na kuamua kiwango cha riba ya Benki Kuu kinachohitajika ili kufikia lengo la mfumuko wa bei unaozingatia ukuaji wa uchumi.

Benki Kuu hutumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha ili kuhakikisha riba katika soko la fedha baina ya mabenki hapa nchini (interbank market rate) inakuwa tulivu sambamba na kiwango cha riba ya Benki Kuu.
Aidha,Benki Kuu hutumia riba za soko la fedha baina ya mabenki, kama lengo la uendeshaji ili kufikia malengo mapana ya kiuchumi.

Katika shughuli zake za kila siku, Benki Kuu hutathimini hali ya ukwasi katika mfumo wa kibenki na kuamua kiasi, muda na aina ya vyenzo zitakazotumika katika usimamizi wa ukwasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here