BoT yasisitiza umuhimu wa kusoma mkataba kabla ya kukopa mkopo


BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kusisitiza umuhimu wa wananchi kuelewa wajibu na haki zao kabla ya kukopa mikopo, huku ikitoa onyo kwa taasisi na watu wanaotoa mikopo bila leseni nchini.
Afisa Sheria Mwandamizi, Idara ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Ramadhani Myonga ameyasema hayo leo Novemba 20,2025 jijini Dodoma katika siku ya pili ya semina kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara.

Semina hiyo ambayo inaratibiwa na BoT imewaleta pamoja waandishi wa habari kutoka mikoa mitano ikiwemo Dodoma, Zanzibar, Dar es Salaam, Morogoro na Pwani.

Bw.Myonga katika semina hiyo alikuwa anawasilisha mada kuhusu namna ya kumlinda mtumiaji wa huduma za fedha (SEMA NA BOT) ambapo amesema kuwa, Benki Kuu imepewa jukumu la kulinda watumiaji wa huduma za kifedha.
Amesema, watumiaji wa huduma za kifedha hulindwa ili kuongeza imani na uaminifu wao katika kutumia huduma na mifumo ya kifedha nchini.

Pia, amebainisha kuwa, imani na uaminifu vinaweza kufikiwa kupitia uwazi wa taarifa, ulinzi wa taarifa za wateja, utoaji wa huduma kwa haki, utaratibu wa kusikiliza malalamiko kwa ufanisi na njia za kusuluhisha migogoro pamoja na utoaji wa elimu na uelewa wa masuala ya fedha.
"Tunapoongelea ulinzi wa watumiaji wa huduma za kifedha tunamaanisha watoa huduma kuzingatia kanuni,taratibu,miongozo na sera ya fedha, hizi zinasimama kama nguzo za mtumiaji wa huduma za fedha."

Amesema kuwa, taasisi za fedha ni eneo pekee ambalo ndilo chachu ya kumuwezesha mwananchi kujiletea maendeleo, hivyo kila mmoja anapaswa kuwajibika ili kuhakikisha mikopo inayotolewa inakuwa kichocheo cha shughuli za maendeleo na si kuwaumiza.
Pia, amesema kila mkopaji anapaswa kupewa nakala ya mkataba wa mkopo kabla na baada ya kusaini.

Amesema, mkataba huo lazima uoneshe masharti yote, muda wa marejesho, adhabu zitakazotumika, pamoja na haki na wajibu wa pande zote.

"Hivyo, lazima kuwepo uwazi na usawa. Mteja, unapokwenda kukopa mkopo katika taasisi za kifedha hakikisha kabla ya kuingia mkataba, uusome na lazima ujue wajibu wako ni upi na haki yako ni ipi."
Pia, amesema kile unachokopa ndicho kinapaswa kuingia katika mkataba. "Lugha ya mkataba ni mbili, Kiswahili au Kiingereza, mteja halazimishwi kupewa mkataba wa lugha ambayo haielewi,kama hauelewi, achana nao."

Vilevile, amesisitiza kuwa ni lazima mkopaji ahakikishe taasisi anayokopa ina leseni rasmi ya kufanya shughuli za kifedha nchini.

Amesema, kukopa katika taasisi zisizo na leseni kunamuweka mteja kwenye hatari ya kupunjwa, kutishiwa au kutolindwa kisheria.
Bw.Myonga amesema, taasisi za fedha pia zinapaswa kulinda taarifa binafsi na za kifedha za wateja, kwani kutoa taarifa za mkopaji kwa watu wasiostahili bila ridhaa ni kosa kisheria.

Aidha,BoT imeendelea kuwahimiza wananchi kutochukulia mkataba wa mkopo kama karatasi za kawaida, bali kama makubaliano ya kisheria yanayofunga maisha yao ya kifedha kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine, BoT imesisitiza kuwa ni haki ya kila mteja kuuliza maswali, kuomba ufafanuzi, na hata kuchukua muda wa kupitia mkataba akishauriana na mtu anayemwamini kabla ya kusaini ili kufanya maamuzi sahihi.

Bw.Myonga amesema,pia BoT inalinda amana za wananchi kwenye benki na kwa watoa huduma ndogo za fedha kupitia mfumo wa SEMA NA BOT.

Aidha,wananchi wanahimizwa kutoa taarifa kuhusu udanganyifu, malipo ya ziada, riba zisizoeleweka au kukosa taarifa sahihi za mikopo kutoka katika taasisi za kifedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news