Teknolojia ya kisasa itumike katika maombi ya maunganisho ya maji-Mhandisi Mwajuma

MOROGORO-Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri ameelekeza teknolojia ya kisasa itumike katika maombi ya maunganisho mapya ya huduma ya maji ili kuondosha urasimu katika kufikisha huduma ya majisafi kwa wateja nchini.
Amesema hayo mkoani Morogoro akihitimisha mafunzo ya maboresho ya Mfumo Mama wa Utoaji Huduma za Maji Kimtandao (MAJIIS) kwa Wataalam wa Sekta ya Maji.

Amezitaka mamlaka za maji kuondokana na matumizi ya karatasi kwasababu yanasababisha malalamiko na kukaa muda mrefu kabla ya mteja kuhudumiwa.
Mhandisi Mwajuma amesema Wizara ya Maji itafuatilia kwa ukaribu uzingatiaji wa Mkataba wa Huduma kwa Mateja katika maombi ya maunganisho ya wateja ambapo pia taasisi katika Sekta ya Maji zimetakiwa katika mfumo kuweka malengo ya mwaka kwenye mfumo, na kuzingatia taratibu za matumizi.

Amesisitiza kuwa baada ya mafunzo hayo, taarifa zote muhimu za uzalishaji, usambazaji, maunganisho, upotevu wa maji na makusanyo zinapaswa kupatikana moja kwa moja kupitia dashibodi ya MAJIIS na sio vinginevyo.

Mafunzo yamehusisha Wataalam wa Sekta ya Maji kutoka Mamlaka za Maji, Bodi za Maji za Mabonde, Vyombo vya Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSOs), EWURA, Mamlaka ya Maji ya Zanzibar (ZAWA) na Wizara ya Teknolojia ya Habari.
Mfumo wa MAJIIS ulianza kutumika mwaka 2020 ukiwa na lengo la kuunganisha mifumo yote ya mapato ya mamlaka za maji na kusimamia kwa pamoja huduma za maji nchini na mwaka 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliuzindua rasmi mfumo huo wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Maji yaliyofanyika Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Maboresho katika mfumo wa MAJIIS yanajumuisha kuanzishwa kwa Moduli ya Uzalishaji Maji, Portal ya Maombi ya Maunganisho Mapya ya Huduma za Maji, utambuzi wa maji yanayopotea pamoja na utengenezaji wa dashibodi ya MAJIIS ili kufuatilia kwa karibu utendaji wa Mamlaka za Maji zipatazo 85, CBWSOs 950 na Bodi za Maji za Mabonde tisa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news