BoT yazidi kuhimiza malipo kidijitali,njia rahisi yenye faida lukuki kwa wananchi na Taifa

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema, kuongezeka kwa matumizi ya mifumo ya malipo kwa njia za kidijitali kutachangia kwa kiasi kikubwa kulinda ubora wa noti za Tanzania na kupunguza gharama zinazotumika katika uchapishaji wa noti mpya.
Afisa Mwandamizi wa BoT,Bw.Atufigwege Jampion Mwakabalula ameyasema hayo leo Novemba 21,2025 jijini Dodoma wakati akitoa mada ya namna ya kutambua alama za usalama katika noti katika semina kwa waandishi wa habari za uchumi na biashara nchini.

Semina hiyo ya siku tatu imeratibiwa na BoT ambapo imewajumuisha waandishi wa habari kutoka mikoa mitano ya Dodoma,Zanzibar, Pwani,Morogoro na Dar es Salaam.

Amesema,matumizi ya fedha taslimu huwafanya wananchi kuwa na uhitaji mkubwa wa noti, hali inayosababisha noti kuchakaa kwa kasi.
Bw.Mwakabalula amebainisha kuwa, kuongezeka kwa matumizi ya malipo ya kielektroniki ikiwa ni pamoja na miamala ya simu, huduma za benki mtandaoni na kadi kutapunguza mzunguko wa noti na hivyo kuongeza uimara wake.

Aidha, amesema hatua hii ni muhimu katika kupunguza matumizi ya serikali kwa kupunguza hitaji la kuchapisha noti mpya mara kwa mara, jambo ambalo linahitaji fedha nyingi kutokana na teknolojia ya usalama inayotumika katika uzalishaji wa noti hizo.

Noti za Tanzania zimegawanyika kuanzia shilingi 500, 1000, 2000, 5000 na 10000 ambapo Afisa Mwandamizi huyo amefafanua kuwa, miongoni mwa changamoto zinazosababisha kuchakaa ni pamoja na matumizi mabaya ambayo yanajumuisha kuziweka katika hali ya unyevu,kuzikunja,kuzibana kwa pini na kuziandika.

Ametaja miongoni mwa njia za kutunza noti hizo kuwa ni kuziweka katika pochi au sehemu ambazo hazitakuwa na mikunjo.
Katika hatua nyingine, Bw.Mwakabalula amesema, miongoni mwa njia za kutambua noti halali ni kuichunguza kwa kuipapasa ili kuhisi mparuzo kwenye maneno yaliyoandikwa kwa maandishi maalumu yanayoonesha thamani halisi ya fedha.

Vilevile,amewasisitizia kuwa, mwananchi anaweza kuitambua noti halali kwa kuangalia sura ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere inayoonekana unapoimulika noti kwenye mwanga maalumu.

Pia kukagua utepe maalumu kwenye noti za shilingi 500, 1000, 2000, 5000 na 10,000 unaoonekana kama madirisha yenye umbo la almasi ambapo hubadilika badilika noti inapogeuzwa geuzwa.

Wakati huo huo, amesema mtu yeyote atakayekutwa na noti bandia au anayejihusisha na utengenezaji wa pesa hizo anakabiliwa na adhabu kali ikiwemo kifungo cha maisha kwa mujibu wa sheria za nchi.
Amesema,pale ambapo unashuku umepewa noti bandia au unamfahamu mtu anayejihusisha na uovu huo unaweza kuwasilisha taarifa zako benki au kwa vyombo vya ulinzi na usalama.

Mbali na hayo, Bw.Atufigwege amesema,Benki Kuu inaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya njia sahihi za kutambua noti halisi.

Amesema,elimu hiyo imelenga kuongeza uelewa wa wananchi ili kuepusha madhara ya kifedha yanayoweza kujitokeza iwapo watu wenye nia ovu wataingiza noti bandia katika mzunguko.

Amesema kuwa, wananchi wanapaswa kuwa makini zaidi wakati wa kupokea fedha, hususan katika maeneo ya biashara zenye mikusanyiko mikubwa.

"Hivyo,kinachotakiwa ni uelewa wa kuzitambua," amesema Bw.Atufigwege huku akiwataka wafanyabiashara na wananchi wasipuuze hatua za ukaguzi wa noti katika shughuli zao za kila siku.
Ikumbukwe kuwa, Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 inatoa mamlaka kwa Benki Kuu pekee kutengeneza na kutoa fedha (noti na sarafu) kwa matumizi nchini Tanzania.

Aidha,hiyo ndiyo fedha halali kwa ajili ya malipo nchini Tanzania. Hivyo, Benki Kuu ina wajibu wa kubuni na kuagiza noti na sarafu ili kukidhi mahitaji ya fedha nchini.

Benki Kuu inahakikisha kwamba sarafu yake ina ubora unaokubalika kwa sarafu nzuri ambao ni kukubalika na umma kama fedha kwa ajili ya kufanya malipo ya bidhaa na huduma.

Pia,fedha hiyo inajumuisha alama za usalama ambazo zinafanya iwe vigumu kutengeneza noti na sarafu zisizo halali na uwezo wa sarafu kudumu kwa muda mrefu.
Ili kutekeleza na kuhakikisha kwamba hali inakuwa hivyo, Benki inatekeleza Sera ya Fedha Safi ambayo inatoa elimu kwa umma kupitia programu mbalimbali zikiwemo semina, maonesho, warsha na vyombo mbalimbali vya habari nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news