Wanafunzi 4,000 wa Mwaka wa Kwanza katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) waanza rasmi safari ya masomo

DODOMA-Zaidi ya wanafunzi 4,000 wa Mwaka wa Kwanza katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) wameanza rasmi safari yao ya masomo kupitia Semina Elekezi iliyoanza Novemba 20, 2025 katika Ukumbi wa Chimwaga.
Katika semina hiyo, washiriki walipata fursa ya kujadili mada mbalimbali zinazolenga kujenga na kuimarisha utamaduni chanya wa kitaaluma na maadili ndani ya mazingira ya chuo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi, Bi. Rhoda Aroko, aliwasihi wanafunzi kutumia muda wao kwa mambo yenye tija na kujiwekea malengo mahsusi yatakayowawezesha kufanikiwa katika masomo yao.

Kwa upande wake, Mlezi wa Wanafunzi kutoka Ndaki ya Insia na Sayansi za Jamii, Bw. Hafidh Abubakar, aliwahimiza wanafunzi kuwa na nidhamu, akisisitiza kuwa tabia hiyo itawasaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali watakazokutana nazo katika safari yao ya kitaaluma.

Naye, Rais wa Serikali ya Wanafunzi (UDOSO), Bi. Jackline Humbaro, aliwakumbusha wanafunzi kuzingatia maadili ya Chuo kwa kuepuka vishawishi na tabia hatarishi zinazosababisha baadhi ya wanafunzi popote duniani kuingia kwenye uraibu na kupoteza mwelekeo.

Semina Elekezi inaendelea kuwa dira muhimu katika kujenga kizazi chenye uelewa mpana, maadili thabiti, na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Semina hii inatarajiwa kuendelea kesho kwa kushirikisha Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news