MWANZA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, amewataka wahitimu wa Chuo cha Benki Kuu ya Tanzania kudumisha uadilifu, uzalendo na ubunifu wanapoanza safari zao katika sekta ya fedha.
Akizungumza katika Mahafali ya Nne ya Chuo hicho yaliyofanyika leo tarehe 28 Novemba 2025, ambako alikuwa Mgeni Rasmi, Gavana Tutuba alisisitiza kuwa sekta ya fedha ni moyo wa uchumi wa taifa hivyo inahitaji watu wenye maadili makubwa na ujuzi wa hali ya juu.
Akizungumza katika Mahafali ya Nne ya Chuo hicho yaliyofanyika leo tarehe 28 Novemba 2025, ambako alikuwa Mgeni Rasmi, Gavana Tutuba alisisitiza kuwa sekta ya fedha ni moyo wa uchumi wa taifa hivyo inahitaji watu wenye maadili makubwa na ujuzi wa hali ya juu.Gavana Tutuba aliwaonya wahitimu dhidi ya kushiriki vitendo visivyozingatia maadili kama wizi, udanganyifu na kusababisha mikopo chechefu, akibainisha kuwa BoT itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa wafanyakazi wa sekta ya fedha nchini na haitasita kuchukua hatua kali kwa wale watakaokiuka maadili ya kazi.
Aidha, aliwahimiza wahitimu kuwa wabunifu, wachapakazi na kutumia maarifa waliyoyapata kujiajiri au kutafuta fursa mpya katika soko la ushindani.Alisema dunia ya sasa inahitaji watu wanaoweza kuwaza nje ya mifumo ya kawaida na kutumia ujuzi wa vitendo (competency-based learning) kuleta mabadiliko chanya katika sekta mbalimbali.
Katika hotuba yake, Gavana Tutuba pia alisisitiza umuhimu wa wahitimu kuendelea kujiendeleza kitaaluma kwa kuwa mabadiliko ya teknolojia na maarifa yanakwenda kwa kasi. Alisema kuhitimu sio mwisho wa safari bali ni hatua ya kwanza ya safari ndefu ya kujifunza.
Akizungumza awali, Mkuu wa Chuo cha Benki Kuu, Dkt. Nicas Yabu, alisema kuwa Chuo hicho kinaendelea kuwa kitovu cha mafunzo ya kikanda ambapo katika mwaka 2024/25, jumla ya washiriki 127 walitoka nje ya nchi ikiwemo Kenya, Uganda, South Sudan, Somalia, Burundi, Zambia, Zimbabwe, Comoros, Botswana na Ghana.
Uwepo wa washiriki hao wa kimataifa uliingizia Benki Kuu dola za marekani 93,500, hatua inayodhihirisha ukuaji na mvuto wa programu za mafunzo zinazotolewa na chuo hicho.
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 36 walitunukiwa Stashahada ya Uendeshaji na Usimamizi wa Benki, huku wahitimu 31 wakitunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Uongozi wa Benki.



