ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo tarehe 22 Novemba 2025, amewaapisha Makatibu Wakuu na Naibu Makatibu Wakuu aliowateua hivi karibuni na kuwataka waache kukaa maofisini, badala yake washuke chini kuwa karibu na wananchi ili kuwahudumia ipasavyo.
Hafla hiyo imefanyika katika Viwanja vya Ikulu, Mkoa wa Mjini Magharibi, na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kuwa utekelezaji wa majukumu ya Watendaji hao Wakuu unatakiwa kuongozwa na mambo matano muhimu:
1. Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2025–2030 kwa kuandaa Mpango Kazi wa kuitekeleza,
2. Hotuba ya Ufunguzi wa Baraza la Wawakilishi,
3. Mpango Kazi wa utekelezaji wa Ahadi za Kampeni,
Amesema nyenzo hizo ndizo dira kuu za utendaji kazi Serikalini na zinapaswa kuongoza hatua zote za kupanga, kusimamia na kutekeleza majukumu ndani ya Wizara na Taasisi za Serikali.
Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amewataka viongozi hao kuzingatia misingi miwili muhimu ya utendaji katika maeneo yao ya kazi ambayo ni Usimamizi Bora wa Utawala na Usimamizi Bora wa Fedha, akisisitiza uongozi wenye kuondoa makundi na kuweka mbele maslahi ya wananchi.
Akigusia masuala ya fedha, Rais Dkt. Mwinyi amewataka kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma kwa kuepuka gharama zisizo na tija na kuongeza juhudi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali, ili kuwezesha utekelezaji madhubuti wa miradi ya maendeleo.
Rais Dkt. Mwinyi amewahakikishia watendaji hao kuwa iwapo watasimamia kikamilifu miongozo aliyoitoa na kufanya kazi kwa kasi na umakini, Serikali itaweza kutekeleza miradi ya maendeleo na kutimiza matarajio ya wananchi kwa kiwango cha juu zaidi.
Amesema nchi inahitaji kasi mpya ya utekelezaji, hivyo kila kiongozi anapaswa kuendana na mwelekeo huo kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Aidha, amesisitiza kuwa Afisi ya Rais iko wazi kupokea ushirikiano, maoni na ushauri wowote utakaosaidia kuboresha utendaji wa Serikali.














