NA DIRAMAKINI
KAMPUNI ya iTrust Finance imezindua mfuko wa kwanza wa uwekezaji wa iTrust East African Community Large Cap Exchange Traded Fund (IEACLC-ETF) wa pamoja utakaoorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) wenye uwekezaji wa kikanda ili kupanua fursa za uwekezaji kwa Watanzania.
Bidhaa hiyo ya kwanza ya aina yake inawawezesha wawekezaji wa ndani na nje kupata fursa ya moja kwa moja kumiliki hisa katika kampuni kubwa, imara na zenye rekodi nzuri katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).Mfuko huo umezinduliwa leo Novemba 18,2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Utafiti,Sera na Mipango kutoka Mamlaka ya Masoko, Mitaji na Dhamana (CMSA), Alfred Mkombo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka.
Amesema, tukio hilo ni la kihistoria na lina mchango mkubwa zaidi katika maendeleo na ustawi wa masoko ya mitaji hapa nchini.
Amesema,huo ni mfuko wa kwanza ambao umeorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam ili kutoa fursa za wawekezaji kununua vipande vya uwekezaji na kuongeza ukwasi katika soko la hisa na kupanua ushiriki wa uwekezaji katika kuongeza mitaji.
Amesema,lengo la kampuni hiyo ni kuwekeza katika hisa za makampuni makubwa yenye mitaji mikubwa na utendaji nzuri na kutoa fursa za uwekezaji kwa wananchi na kwamba ili kufikia malengo ya uwezeshaji kiuchumi ni vyema wananchi kutumia fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwekeza kwenye bidhaa na masoko ya mitaji.
Aidha,ameipongeza Kampuni ya iTrust kwa ubunifu wao ambao utatoa mchango mkubwa katika kufikia Malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 na kwamba mfuko huo una faida kubwa na una lenga utekelezaji wa sera ya serikali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi..
Amesema,pia mfuko huo utawezesha miradi toka kwenye sekta mbalimbali kwenye kampuni hizo kufanyika kwa pamoja na wananchi wa kipato cha chini pamoja na kuwezesha wawekezaji kupata faida ya ongezeko la thamanii na kuchochea maendeleo ya uchumi na hivyo kuleta tija.
Amesema,uwekezaji huo unapunguza uwezekano wa kupata hasara kwa kuwa mwekezaji anawekeza katika dhamana mbalimbali katika zaidi ya kampuni 12 hivyo kupunguza uwezekano wa kupata hasara.
Amesema,CMSA ina jukumu la kuendeleza na kusimamia masoko ya mitaji kwa kufuata sheria, taratibu na miongozo ili kuleta haki kwa washiriki wote ambapo katika utekelezaji wa jukumu hilo kampuni hiyo imekidhi matakwa ya kisheria ya uwekezaji wa dhamana za uanzishaji wa mifuko ya dhamana ya pamoja na kufanya kampuni hiyo kuwa na mifuko saba.
Kwa upande wake Mohamed Wasame mmoja wa Wakurungezi wa Kampuni ya iTrust amesema, mfuko huo mpya wa ukanda wa Afrika Mashariki, ambao unawekeza katika kampuni zote kubwa toka Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.
Pia,ETF hii mpya inawawezesha wawekezaji kukuza mitaji yao kwa kununua vipande vinavyowakilisha hisa za kampuni bora na kubwa (large-cap) zilizoorodheshwa katika Masoko ya Hisa ya Dar es Salaam (DSE), Nairobi (NSE), Uganda (USE), na Rwanda (RSE) ambapo unaongozwa na kielelezo mchanganyiko kinachojumuisha faharisi za masoko yote manne, hivyo kutoa uwekezaji mpana na wa aina mbalimbali kwa ulinganifu wa juu.
Aidha,katika kipindi cha Mauzo ya Awali ya Umma (IPO) kinachoanza tarehe 17 Novemba hadi 12 Desemba,mwaka huu wawekezaji wanaweza kushiriki kwa kuanzia kiwango cha chini cha shilingi 100,000, hatua inayoufanya uwekezaji huu kufikiwa kwa urahisi na wawekezaji wapya pamoja na wale wenye uzoefu mkubwa.
Baada ya kuorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, vipande vya ETF vitauzwa na kununuliwa moja kwa moja sokoni kwa bei itakayokuwa inatumika wakati huo.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa iTrust Finance, Faiz Arab, amesema kuwa, IEACLC-ETF ni hatua muhimu katika safari ya kukuza na kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini.
“ETF hii inafungua ukurasa mpya kwa wawekezaji nchini Tanzania,” amesema Bw. Arab.
“Kwa mara ya kwanza, mtu mmoja mmoja ataweza kufikia mfuko wa kikanda unaosimamiwa kitaalam kupitia bidhaa rahisi na nafuu.Afrika Mashariki ni moja ya kanda zinazokua kwa kasi barani, na tunajivunia kuwapa wateja wetu njia rahisi ya kunufaika na ukuaji huo.
"Lengo letu ni kuondoa vikwazo vya uwekezaji ili kila mtu, mzoefu au anayeanza, aweze kushiriki katika mafanikio ya kiuchumi ya ukanda huu na kwamba ETF hii ni kwa ajili ya wawekezaji wanaolenga kujenga utajiri wa muda mrefu na walio tayari kuwekeza katika masoko ya hisa.
Kwa kuwekeza kwenye mkusanyiko wa kampuni kubwa na thabiti katika sekta mbalimbali, mfuko unapunguza hatari ya kuegemea upande mmoja na kuongeza nafasi ya kupata faida endelevu kadiri thamani ya hisa inavyoongezeka.
Ukuaji wa uchumi wa kikanda na kuimarika kwa matokeo ya kampuni kunatarajiwa kuongeza thamani ya hisa hizi kwa muda.
Arab amesema kuwa, muundo wa mfuko umezingatia uwazi na ulinzi kwa wawekezaji.
IEACLC-ETF inasimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), huku Benki ya NBC ikifanya kazi kama mwangalizi wa mali za wawekezaji.
iTrust Finance itakuwa ikichapisha taarifa ya thamani halisi ya mfuko (NAV) kila siku, pamoja na taarifa za mgawanyo wa mali kila wiki na taarifa kamili za mfuko kila mwezi ili kuhakikisha uwazi na ufuatiliaji rahisi wa uwekezaji.Aidha,ili kuwekeza, mteja mpya anachotakiwa ni kufungua akaunti kupitia tovuti ya iTrust Finance, www.itrust.co.tz, kwa kujaza fomu ya kidijitali na kuwasilisha nyaraka za utambulisho (KYC).
Kwa wale ambao tayari ni wateja wanaweza kujaza fomu ya ETF IPO inayopatikana mtandaoni.
Baada ya usajili kukamilika, mwekezaji atapokea baruapepe ya “karibu” yenye maelezo ya akaunti ya benki kwa ajili ya kufanya malipo.
Mara tu malipo yakikamilika, mwekezaji atathibitishiwa kwa kutuma risiti kwa barua pepe ya customerservice@itrust.co.tz.
Uzinduzi wa IEACLC-ETF unakuja kipindi ambacho Watanzania wengi wanatafuta njia za uwekezaji zilizo za kisasa, zenye mgawanyo mpana na zilizopo nje ya mifumo ya jadi ya akiba.
Kupitia chombo hiki kimoja cha uwekezaji ambacho ni rahisi kukiingia na kutoka, iTrust Finance inalenga kujenga kizazi kipya cha wawekezaji walioelimika, walio tayari kunufaika na fursa za kikanda.





















