DODOMA-Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo pamoja na Naibu wake Mhe. Kasper Mmuya, leo Novemba 18, 2025 wamewasili rasmi ofisi za Wizara ikiwa ni mara tu baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa huo.
Viongozi hao wawili walipokelewa kwa furaha na menejimenti, viongozi wa taasisi zilizo chini ya wizara pamoja na watumishi wa makao makuu ambapo Waziri Mhe.Dkt Leonard Akwilapo amemshukuru Rais kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuiongoza wizara hiyo.
Amepongeza pia tukio la kikao cha kwanza cha utambulisho, akisisitiza kuwa sasa ni wakati wa kushirikiana kwa karibu na kutekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa.
“Mheshimiwa Rais amesisitiza kazi, utu na maendeleo. Tufanye kazi kwa moyo, kwa kufuata taratibu za huduma bora kwa wateja, kwa ubora uleule na ndani ya muda unaotakiwa,” amesema Dkt. Akwilapo.
Aidha, amekumbusha umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia staha, kujali muda na kutoa huduma zenye tija kwa taifa.



