Mabaki ya mwili wa Mtanzania, Joshua Loitu Mollel aliyeuawa kusini mwa Israel kurejeshwa nchini

DODOMA-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema kwamba mamlaka za Israel zimethibitisha kuwa mabaki ya mwili yaliyokabidhiwa kwa Serikali ya Israel hivi karibuni kutoka Gaza ni ya Bw. Joshua Loitu Mollel, Mtanzania mwenye umri wa miaka 21 aliyekuwa mwanafunzi wa mafunzo kwa vitendo ya kilimo (intern) aliyeuawa wakati wa mashambulizi ya tarehe 7 Oktoba 2023 kusini mwa Israel na mwili wake kuchukuliwa na kupelekwa Gaza.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 8,2025 huku ikielezea kuwa, hii ni taarifa njema na imekuwa ni ya faraja kubwa kwa familia na Taifa kwa ujumla.

"Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mjini Tel Aviv unaendelea kushirikiana na Serikali ya Israel kukamilisha mchakato wa urejeshwaji wa mwili nchini.

"Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inashirikiana kwa karibu na familia katika kufanikisha mapokezi ya mwili pamoja na mazishi ya heshima kwa kijana wetu.

"Kwa mara nyingine tena, Wizara inatoa pole za dhati kwa familia ya Mollel na kwa Watanzania wote walioathirika na msiba huu."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news