Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Lake Oil Group, Stephen Mtemi, ameeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha watu kuchoma vituo vya mafuta vya kampuni hiyo, akisema mbali na hasara kubwa iliyotokea, Watanzania zaidi ya 300 waliokuwa wakifanya kazi kwenye vituo hivyo sasa wako nyumbani bila kazi.
Amesema kampuni hiyo ina wafanyakazi takribani 8,000, huku asilimia kubwa wakiwa Watanzania. Katika vituo takribani 38 vilivyochomwa moto Tanzania nzima, Mtemi amesema vilikuwa na wafanyakazi zaidi ya 300 ambao kwa sasa wamepewa likizo bila malipo.
“Kwa habari tulizozisikia mitandaoni na mitaani, watu wengi wanahusisha Lake Oil na wanasiasa. Inaelezwa kuwa hilo ndilo lilisababisha washambuliaji kufanya vurugu na kuharibu mali kwa lengo la kuwafikia wanasiasa,” amesema.
Amefafanua kuwa kampuni ya Lake Oil ni mali ya Mtanzania mzawa anayeitwa Ally Adha Awadhi, na kwamba hana uhusiano wa aina yoyote na wanasiasa wanaotajwa, wala hawana umiliki wowote ndani ya kampuni hiyo.
Amesema si haki kwa wananchi kuharibu mali ya Lake Oil kwa kudhani inamilikiwa na wanasiasa, kwani hatua hiyo inaathiri maisha ya wafanyakazi pamoja na mmiliki wa kampuni.
Hata hivyo, Mtemi ametoa pole kwa wananchi wote walioathirika kwa namna moja au nyingine na vurugu zilizoibuka kufuatia uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo



























