Matarajio chanya Sekta ya Madini Tanzania, Rais Dkt.Samia abainisha mengi

NA DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema,sekta ya madini imeendelea kuwa kinara katika kuchangia makusanyo ya Serikali, pato la wananchi na uwekezaji kwenye huduma za kijamii kama elimu na afya, hatua iliyochochewa na ongezeko la mchango wake kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi 10.1 mwaka 2024.
Ameyasema hayo leo Novemba 14, 2025, wakati akihutubia kwenye ufunguzi wa Bunge la 13 jijini Dodoma.

Rais Dkt.Samia ameeleza kwamba, mageuzi na mikakati mipya imeiweka Tanzania kwenye mwelekeo thabiti wa kuwa kitovu cha biashara ya madini Afrika Mashariki na Kati ifikapo mwaka 2030.

"Tanzania imebarikiwa sana na madini ya aina mbalimbali. Hadi sasa, eneo lililopimwa na kufanyiwa utafiti wa kina ni asilimia 16 tu ya eneo lote lenye miamba yenye madini nchini.

Kazi yetu miaka inayokuja ni kuhakikisha madini haya yanawaletea maendeleo wananchi na kuwainua kiuchumi.
Katika kipindi kilichopita, tuliweza kuongeza mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 10.1 mwaka 2024.

Hatua hii inamaanisha madini yanachangia zaidi mapato kwa wananchi, makusanyo kwa Serikali, na uwekezaji kwenye huduma za kijamii.

Kuelekea mwaka 2030, tutakamilisha Mkakati wa madini adimu (critical minerals) ili Serikali itambue aina ya madini, viwango vya madini na eneo madini yalipo.

Kwa kuwa Madini ya Kimkakati ndio yanayohitajika zaidi Duniani, tutaongeza umakini katika kusimamia uwekezaji wa madini hayo.

Katika jitihada zetu za kuendeleza sekta hii ya madini, tutapitia upya leseni zilizotolewa ili kubaini leseni ambazo hazijaendelezwa na kuchukua hatua za kuzitoa kwa wachimbaji wenye nia ya dhati ya kufanya uendelezaji wa maeneo husika.

Wachimbaji wadogo wamekuwa nguzo ya kutegemewa katika sekta ya madini nchini. Hivyo basi, tutatenga maeneo maalum kwa ajili yao, tutawapatia leseni na tutawaendeleza kwa kuwapa mitaji na mitambo ya uchorongaji, pamoja na kuwapatia taarifa sahihi za kijiolojia.
Aidha, tutaendeleza utaratibu wa Benki Kuu kununua akiba ya dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo na wa kati walio na leseni halali kutoka Tume ya Madini.

Tunafanya hivi kuhakikisha wachimbaji wanapata mnunuzi wa uhakika, kupunguza utoroshaji wa madini na pia kurasimisha biashara ya uchimbaji kwa vijana wa Tanzania.

Tutaendelea kuimarisha masoko ya madini na vito. Kipekee kwa madini ya Tanzanite, tunaenda kumalizia jengo la Tanzanite Exchange Centre (TEC) katika eneo la Mirerani.

Mbali na kuwa Nchi yetu ni mzalishaji mkubwa wa madini, tunataka ifikapo 2030 Tanzania iwe kituo kikuu cha uuzaji wa madini yote katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Hatua nyingine muhimu katika kuongeza mchango wa Sekta ya madini katika maendeleo ya nchi ni kusimamia uongezaji wa thamani ya madini hayo hapahapa nchini.
Tunadhamiria kuwa na kiwanda cha kuchenjua madini (multipurpose refinery) ifikapo 2030. Tutaondokana na kusafirisha makinikia kwenda nje ili tuokoe ajira ambazo tumekuwa tukizipoteza.

Vilevile, tutaanzisha Mfuko wa Wakfu wa Madini (Minerals Sovereign Wealth Fund) ili fedha zitokanazo na madini zije ziwafae vizazi vijavyo.

Tunafanya hivyo tukitambua kuwa madini si mahindi kwamba ukiyavuna, utatenga mbegu ili uyaoteshe tena. Ukichimba madini kuna mwisho wake.

Tunataka vizazi vyetu visikute mashimo tu, bali wakute fedha zitokanazo na madini tunayoyavuna leo,"amefafanua kwa kina Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here