Mussa Azzan Zungu ashinda kwa kishindo Spika wa Bunge la Tanzania

NA DIRAMAKINI 

MBUNGE wa Jimbo la Ilala jijini Dar es Salaam, Mussa Azzan Zungu, ameibuka kidedea katika uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiahidi kuongoza chombo hicho kwa uwazi, nidhamu na uwajibikaji mkubwa.
Uchaguzi huo umefanyika jijini Dodoma ambapo Zungu alipata kura 378 kati ya kura zote zilizopigwa na wabunge, hatua iliyomuwezesha kushika rasmi nafasi ya Spika wa Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa ushindi huo, Zungu anakabidhiwa jukumu zito la kusimamia mwenendo wa mijadala, kuhakikisha utekelezaji wa majukumu ya kibunge kwa maslahi ya wananchi, na kudumisha heshima ya Bunge kama mhimili muhimu wa dola.
Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu akivishwa rasmi Joho rasmi la Spika mara baada ya kula kiapo rasmi cha kuwa Spika wa Bunge katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 13 leo Novemba 11, 2025 Dodoma.
Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu ana uzoefu mkubwa katika siasa, kwani mwaka 2005 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Ilala, nafasi aliyoendelea kuishikilia kwa vipindi vitano mfululizo hadi mwaka 2025.

Ndani ya Bunge, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo: Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje (2007-2011), Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wa Jumuiya ya Madola (CPA) -Tanzania, alikuwa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii (2015-2018)

Baadaye akawa Mwenyekiti wa Bunge katika vipindi vya 2012 na 2016. Mwaka 2020, aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), nafasi aliyohudumia hadi mwisho wa kipindi cha Bunge la 12.

Kufuatia kujiuzulu kwa Spika Job Ndugai, Zungu alichaguliwa kuwa Naibu Spika, kabla ya kupanda ngazi hadi kuwa Spika wa Bunge la 13 mwaka 2025.
Mwenyekiti wa Kikao cha Uchaguzi wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Willium Lukuvi akiongoza Kikao hicho wakati wa Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Kwanza wa Bunge la 13 leo Novemba, 2025.
Katika uchaguzi huo, wagombea wengine walioshiriki ni Veronica Tyeah wa NRA, Anitha Mgaya wa NLD, Chrisant Nyakitita wa DP, Ndonge Ndonge wa AAFP, na Amin Yango wa ADC, ambapo kati yao wawili tu walipata kura moja moja huku wengine wakikosa kura kabisa.

Zungu amechaguliwa kwa kura 378 kati ya 383 zilizopigwa kutoka kwa wabunge wa bunge la Tanzania, huku kura 3 zikiharibika.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema uteuzi wa Zungu unaashiria mwanzo mpya wa uongozi wa Bunge unaotarajiwa kuweka msisitizo kwenye uwajibikaji wa Serikali na uwakilishi wenye tija kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news