TELAVIV-Ubalozi wa Tanzania nchini Israel kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel ilifanya hafla ya kuuaga mwili wa Mtanzania Joshua Loitu Mollel, leo, Jumanne, tarehe 18 Novemba 2025, katika Mnara wa Mashujaa, uliopo Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion. 

Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mhe. Sharen Haskel, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Wanadiplomasia, Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel, Watanzania waishio Israel, Waisrael walioguswa na msiba huu na Wanahabari.
Hafla hiyo pia ilirushwa mubashara kutoa fursa kwa wanafamilia na walioguswa na msiba huu kufuatilia tukio hilo.
Katika hotuba yake, Mhe. Balozi Kallua alitoa salamu za rambirambi kwa familia ya Mzee Mollel na Tanzania kwa ujumla kwa kumpoteza kijana Joshua, ambaye alikuwa na ndoto kubwa ya kujishughulisha na kilimo biashara baada ya kumaliza mafunzo yake.
Aidha, Balozi Kallua alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Israel, Jeshi la Israel na wale wote waliopambana bila kuchoka kuhakikisha kuwa mwili wa Joshua na miili ya wahanga wengine wa tukio hilo inarejeshwa nchini Israel.
Vilevile, aliahidi kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na Israel katika kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali kwa manufaa ya pande zote mbili.
Kwa upande wake, Naibu Waziri Haskel alitoa salamu za rambirambi kwa familia ya Mzee Mollel kwa kumpoteza kijana wao, ambaye alikatizwa uhai wake kinyama na kundi la Hamas.Alisikitika kusema kuwa Israel haikuweza kuulinda uhai wa Joshua pamoja na Waisrael wengine zaidi ya 1000 waliopoteza maisha kutokana na uvamizi huo.
Vilevile, alisema kuwa Israel ilitoa umuhimu katika kuhakikisha kuwa mwili wa Joshua unapatikana kama ambavyo ilifanya kwa raia wake, na kwamba ilibidi kubadilishana na wafungwa ili mradi kufanikisha suala hilo.
Naibu Waziri Haskel alitumia fursa hiyo kuahidi kuwa Israel itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha zaidi mahusiano yaliyopo baina ya nchi hizi mbili.
Hotuba zingine zilizotolewa katika hafla hiyo ni pamoja na ya Mkurugenzi wa MASHAV; Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Dawati la Wageni, Mateka na Watu Waliopotea; Mtendaji Mkuu wa Agrostudies; na Mwakilishi kutoka Kibbutz Nahal Oz ambako ndiko alikokuwa anaishi.
Katika hotuba yake Mkurugenzi wa MASHAV, pamoja na kuwasilisha salamu za pole, alitumia fursa hiyo pia kujulisha kuwa taasisi hiyo imeazimia kuanzisha programu maalum katika chuo alichokuwa akisoma Joshua ili kuenzi jitihada na ndoto ya maendeleo aliyokuwa nayo kwa jamii na taifa kwa ujumla.
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa sala iliyoongozwa na Padre Quinbert Salvius Kinunda, Mmishenari wa Afrika kutoka Tanzania.
Kijana Joshua, aliyekuwa na umri wa miaka 21, aliuawa na Kundi la Hamas, tarehe 7 Oktoba 2023, alipovamiwa katika shamba la ng’ombe wa maziwa huko Kibbutz Nahal Oz alipokuwa anafanya mafunzo ya utarajali yanayoratibiwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Israel (MASHAV), chini ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel kupitia taasisi ya Agrostudies.
Baada ya kuuawa, mwili wake ulipelekwa Gaza. Jitihada mbalimbali zilifanyika na serikali yetu pamoja na Serikali ya Israel kuhakikisha kuwa mwili huo unarejeshwa Israel ili upelekwe Tanzania kwa ajili ya mazishi ya heshima.
Tarehe 5 Novemba 2025, mabaki ya mwili yalirejeshwa Israel na kuthibitishwa na mamlaka za Israel kuwa ni ya Joshua. Mazishi yamepangwa kufanyika tarehe 20 Novemba 2025, huko Simanjiro, Manyara. “Bwana ametoa na Bwana ametwaa, jina la Bwana lihimidiwe” Ayubu 1:21





