ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mauzo ya nyumba za kisasa zilizopo Kisakasaka, Wilaya ya Magharibi “B”, nje ya mji wa Zanzibar, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Sultan Said Suleiman wakati akizungumzana waandishi wa habari.
Amesema,uzinduzi huo utafanyika Novemba 22, 2025 kuanzia saa 4:00 asubuhi, na utahudhuriwa na wageni mbalimbali wakiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Amesema, uzinduzi huo utaambatana na kufunguliwa kwa mfumo wa mauzo ya nyumba ambao wafanyakazi na wateja wengine watautumia kupata maelekezo pamoja na vigezo vya ununuzi wa nyumba hizo, ambazo zitauzwa kwa bei tofauti kulingana na aina ya nyumba
Amefafanua kuwa, kwenye uzinduzi huo, ZHC itazindua nyumba za Kisakasaka aina ya D (312 nyumba) na aina ya B (548 nyumba). Katika makazi hayo, kutakuwa na nyumba za bei nafuu zenye vyumba viwili, vitatu na vinne.
Aidha, amesema bei za nyumba hizo zinaanzia shilingi milioni 92, milioni 100, milioni 200 na kuendelea, kutegemea ukubwa na aina ya nyumba.
Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amesema kuwa, kutazinduliwa pia skimu maalum ya mauzo itakayowawezesha wafanyakazi kununua nyumba na kulipa kidogo kidogo kwa muda wa miaka 22, ambapo benki mbalimbali zitakuwepo ili kutoa mikopo kwa wateja wao.
Pia, ZHC itazindua skimu ya ZERO Interest, ambayo ni mahsusi kwa waislamu kukopa bila riba, na marejesho yake yatadumu kwa muda wa miaka mitatu.
Vilevile, shirika hilo litaizindua jarida (magazine) linaloonesha shughuli na mafanikio ya ZHC katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), Sultan Said Suleiman amesema Serikali ina nia ya dhati ya kuwapatia wananchi makazi bora na ya bei nafuu katika wilaya zote za Unguja na Pemba.
Aliyataja baadhi ya maeneo ambayo nyumba mpya zinajengwa kuwa ni Kisakasaka nyumba 1,625.
Kati ya hizo Kisakasaka A ina nyumba 240,Kisakasaka B nyumba 548,Kisakasaka C nyumba 520 na Kisakasaka D nyumba 312.
