DODOMA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kufungua fursa mpya za kijamii na kiuchumi kupitia Sekta ya Utamaduni na Sanaa nchini.
Dkt. Samia ameahidi hayo Novemba14, 2025 jijini Dodoma, wakati akihutubia Bunge la 13, la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo amesema, Utamaduni hususani Lugha ya Kiswahili itaendelea kukuzwa na kupewa thamani zaidi Kimataifa.
"Maendeleo ya nchi yoyote yanaonekana katika Utamaduni na ustaarabu wake isitoshe katika dunia ya leo Tamaduni ni bidhaa na uchumi hivyo tutakuza na kuifanya lugha yetu ya Kiswahili kuwa bidhaa," amesema Rais Dkt. Samia.
Kwa upande wa Sekta ya Sanaa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa, Serikali itaanza ujenzi wa Studio ya filamu ya kisasa ili kupandisha thamani ya kazi ya filamu na kuongeza ajira na uchumi wa nchi.
Vilevile Mhe. Rais ameongeza kuwa Serikali itajenga Ukumbi wa kisasa wa maonesho ili kuwawezesha Wasanii kufanya matamasha ya kimataifa na kuvutia Wasanii wa nje kuja kufanya matamasha hapa nchini.
