NA DIRAMAKINI
WIZARA ya Maliasili na Utalii imewahakikishia wananchi, wadau wa utalii na jumuiya ya kimataifa kwamba hali ya amani na utulivu imerejea nchini Tanzania kufuatia kudhibitiwa kwa vurugu zilizotokea kati ya tarehe 29 Oktoba hadi 1 Novemba, 2025.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Novemba 4,2025 na Nteghenjwa Hosseah, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wizara imesema, shughuli zote za kijamii na kiuchumi zinaendelea kama kawaida katika maeneo yote ya nchi, huku huduma za usafiri na utalii zikiendelea kutolewa kwa utaratibu wa kawaida.
“Tanzania kama mwanachama wa Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) inatekeleza na kusimamia Mwongozo wa Utalii Kimataifa unaoelekeza nchi kuhakikisha usalama wa wageni, ikiwemo wasafiri na watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali wawapo nchini,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, Wizara imefafanua kuwa vituo vyote vya kuingia na kutoka nchini kupitia usafiri wa anga, barabara, maji na reli vinaendelea kutoa huduma bila changamoto yoyote.
Vivyo hivyo, huduma za usafiri wa umma na sekta binafsi za utalii zinaendelea kwa utaratibu wa kawaida na kwa ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na wadau.
Wizara imewahimiza wasafiri na watalii kuendelea na mipango yao ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania bila hofu yoyote, ikisisitiza kuwa nchi bado inaendelea kuwa salama na yenye mazingira rafiki kwa shughuli zote za kiuchumi, uwekezaji na utalii.
“Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kuwa nchi salama, yenye utulivu, na mazingira rafiki kwa shughuli zote za usafiri, uwekezaji kibiashara na utalii; hivyo Serikali inachukua fursa hii kuwakaribisha wageni wote nchini,” imesisitiza Wizara.
