Serikali yapiga marufuku masomo ya ziada wakati wa likizo Desemba

NAIROBI-Serikali ya Kenya imepiga marufuku masomo ya ziada wakati wa likizo ya Disemba,mwaka huu.
Waziri wa Elimu nchini Kenya,Mheshimiwa Julius Migos Ogamba.

Kwa mujibu wa Taifa Leo,uamuzi huo unakuja siku chache baada ya shule kutuma barua kwa wazazi zikiwataka wanafunzi kurejea darasani wiki ijayo baada ya kukamilika kwa mitihani ya Mfumo wa Tathmini ya Elimu ya Msingi ya Kenya (KPSEA) na Mfumo wa Tathmini ya Elimu ya Sekondari ya Kati Kenya (KJSEA).

Mtihani wa KPSEA ulimalizika wiki iliyopita huku ule wa KJSEA ukikamilika Novemba 3, 2025.

Waziri wa Elimu nchini Kenya,Mheshimiwa Julius Migos Ogamba amesema, shule haziruhusiwi kufanya masomo ya ziada wakati wa likizo.

“Ni kinyume cha sheria kufanya masomo ya ziada baada ya shule kufungwa. Tutatoa onyo rasmi kuhusu hilo kwenye barua zitakazosambazwa shuleni.

"Maafisa wetu wa elimu walioko mashinani watafanya ukaguzi ili kuhakikisha hakuna shule inayoendelea na masomo wakati wa likizo,” alisema Bw.Ogamba kwenye mahojiano na Taifa leo Dijitali.

Wiki iliyopita, Muungano wa Wazazi Nchini Kenya (NPA) ulitoa tahadhari kufuatia taarifa kwamba shule kadhaa nchini humo zimetuma barua kwa wazazi kuwajulisha kuhusu masomo ya ziada.

Kwa mujibu wa muungano huo, baadhi ya shule za msingi na sekondari zimetuma barua kwa wazazi kuwatayarisha watoto wao kwa masomo ya ziada wakati wa likizo ya Disemba.

Aidha, mwenyekiti wa muungano huo, Bw.Silas Obuhatsa alisema, wazazi pia wameagizwa kulipa ada ya masomo hayo ambayo yataanza rasmi wiki ijayo baada ya kumalizika kwa mitihani ya kitaifa ikiwemo KPSEA, KJSEA na ile ya kidato cha nne (KCSE).

Obuhatsa alisema, wazazi kutoka sehemu mbalimbali nchini wamejulisha ofisi yake kuhusu uhalifu huo akiitaka wizara kuwachukulia hatua kali za kisheria shule hizo.

“Shule kadhaa zimewaagiza wazazi kuanza kulipa ada ya masomo ya ziada kuanzia Jumanne wiki ijayo, wakilenga wanafunzi wa Gredi ya 1 hadi 9 yakipangwa.

"Shule nyingi zimeamua kutofunga kulingana na kalenda ya elimu. Badala yake, zimepanga kuendelea na masomo mara tu baada ya mitihani kumalizika,” alisema Bw.Obuhatsa.

Aliwatuhumu walimu wakuu ambao wamepanga masomo hayo akisema wanatamaa ilhali wanalipwa mishahara.

Wiki mbili zilizopita,wabunge walimtaka Waziri Ogamba kutoa maagizo makali kwa shule kuhakikisha zinafuata maagizo ya wizara.

Hii ni kufuatia malalamiko kutoka kwa wazazi na wadau wa elimu kwamba baadhi ya wanafunzi, wakiwemo watoto wadogo wa miaka saba, wanalazimishwa kwenda shuleni alfajiri ya saa kumi.

“Shule zikikaidi maagizo ya wizara, hatua kali za kisheria zichukuliwe,” alisema Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Kisii, Bi Dorice Donya.

Aliitaka wizara kushirikiana na Wizara ya Usalama wa Ndani kuhakikisha maagizo yanatekelezwa na shule zitakazokaidi zinachukuliwa hatua kali.(Taifaleo)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news