NA DIRAMAKINI
KLABU ya Simba (Simba Sports Club) ya jijini Dar es Salaam imeendelea kukumbana na wakati mgumu katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika baada ya kupoteza mechi kwa mara ya pili mfululizo.
Leo Novemba 30,2025 imelala kwa mabao 2-1 dhidi ya wenyeji Stade Malien kwenye Uwanja wa Machi 26,Bamako nchini Mali.
Katika mchezo huo uliokuwa mkali kwa vipindi vyote viwili, wenyeji Stade Malien waliuanza mchezo kwa kasi na kupata mabao mawili ya haraka kupitia Taddeus Nkeng Fomakwang (Nkeng) dakika ya 16 na lsmaila Simpara dakika ya 23, na kuiweka Simba katika wakati mgumu mapema.
Aidha,kipindi cha pili kilishuhudia Simba ikirejea kwa nguvu ikitafuta kurekebisha makosa, na jitihada zao zilizaa matunda dakika ya 54 baada ya Mshambuliaji Neo Maema kufunga bao pekee la Wekundu wa Msimbazi. Hata hivyo, juhudi hizo hazikutosha kuirejesha Simba kwenye mchezo.
Matokeo hayo yanaifanya Simba SC kuendelea kushika mkia wa Kundi D bila alama baada ya michezo miwili. 

Petro Atletico wanaongoza kundi hilo kwa pointi 4, wakifuatiwa na Stade Malien wenye pointi 4 pia, huku Esperance de Tunis wakishika nafasi ya tatu kwa pointi 2.
Hata hivyo,Simba sasa inalazimika kuongeza umakini na kupata ushindi kwenye michezo ijayo endapo inataka kufufua matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
