NA DIRAMAKINI
SIMBA Sports Club (Simba SC) ya jijini Dar es Salaam imechukua alama tatu muhimu ugenini baada ya kuichapa JKT Tanzania mabao 2-1.
Ushindi huo wa mtanage wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara umepatikana Novemba 8,2025 katika dimba la Meja Jenerali Isamuhyo lililopo Mbweni jijini Dar es Salaam.
Katika mtanage huo,mshambuliaji wa JKT Tanzania, Edward Songo dakika ya 60' aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuzigusa nyavu za klabu ya Simba msimu huu.
Bao hilo ambalo lilitaka kuvuruga mipango ya Simba SC ambapo dakika 45 za kwanza walitoshana nguvu,Wilson Nangu dakika ya 63' alifunga bao ambalo lilirejesha matumaini mapya.
Dakika ya 77 ya mchezo huo, Jonathan Sowah alifunga hesabu kwa bao ambalo liliwakatisha tamaa wazee wa Mapigo na Mwendo
Simba SC imerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara ikifikisha alama 9 baada ya mechi tatu huku JKT Tanzania ikisalia nafasi ya 7, alama 7 baada ya mechi 6.
Aidha, nafasi ya pili inashikiliwa na Pamba Jiji yenye alama 9 huku Mbeya City ikiwa nafasi ya tatu kwa alama 8.

