Tanzania yaihakikishia Dunia hali ya utalii iko salama

RIYADH-Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, akiongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 26 wa Baraza Kuu la Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kilichoanza Novemba 9, 2025, jijini Riyadh, Saudi Arabia, ameihakikishia dunia kuwa hali ya utalii na amani viko imara nchini Tanzania kufuatia machafuko yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi katika baadhi ya maeneo.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo wakati akichangia Taarifa ya Utekelezaji ya Mwaka ya Taasisi hiyo ambapo pia Tanzania ilinufaika na programu mbalimbali ikiwemo kuandaa Mkutano wa Dunia Kanda ya Afrika wa Utalii wa Vyakula uliofanyika Arusha April mwaka huu na kufadhiliwa baadhi ya programu za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya Safu za Milima ya Usambara.

“Mheshimiwa Mwenyekiti wa Baraza hili baada ya kumpongeza Katibu Mkuu na Sekretarieti ya UN Tourism kwa utekelezaji ambao Tanzania pia imenufaika, naomba kutumia fursa hii kutoa taarifa kuwa Tanzania ni salama baada ya kadhia iliyojitokeza wakati wa uchaguzi.
“Serikali imefanya jitihada na kurejesha nchi yetu katika hali ya utulivu na hivyo kuendelea kuwa salama kwa watalii na vivutio vyetu vyote mnavyovijua viko salama. Nawakaribisha wajumbe wa mkutano huu na wadau wengine wa utalii kuja na kuendelea kutembelea nchi hii ambayo ni kivutio bora Afrika kwa utalii wa safari,” alisema Dkt. Abbasi.

Aidha, mbali ya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 32 pekee kati ya wanachama wa Umoja huo wanaofikia 160 kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji (Executive Committe), leo pia Baraza Kuu hilo limeipitisha Tanzania kuwa Mjumbe wa Kamati ya Kuhakiki wanachama (UN Tourism Credentials Committe).
Mkutano huo unaendelea jijini hapa na pamoja na mambo mengine utajadili kuhusu matumizi ya akili mnemba katika kutangaza utalii na pia jioni hii umemthibitisha Sheikha Nasser Al Nowais kutoka UAE kuwa Katibu Mtendaji mpya wa taasisi hiyo muhimu kwa sekta ya utalii duniani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news