NA DIRAMAKINI
MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa taarifa kuhusu kuongezeka kwa viwango vya joto katika maeneo mbalimbali nchini, hususan yale yenye misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
Ongezeko hilo limejitokeza katika kipindi cha miezi ya hivi karibuni kutokana na kusogea kwa Jua la Utosi pamoja na upungufu wa mvua katika maeneo husika.
Kwa mujibu wa TMA, vipindi vya Jua la Utosi hufikia kiwango cha juu mwishoni mwa Novemba wakati jua linapoelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni), na hali hii hurudiwa tena Februari jua linapoelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
Kipindi hiki huambatana na mionzi mikali ya jua inayopelekea ongezeko la joto, kwani uso wa Dunia huwa karibu zaidi na Jua katika eneo husika.
"Kwa kawaida vipindi vya Jua la Utosi nchini hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati Jua la Utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati Jua la Utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa).
"Jua la Utosi huambatana na hali ya ongezeko la Joto kwa sababu uso wa Dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na Jua kuliko maeneo mengine."
Takwimu zinaonesha kuwa,katika kipindi cha mwezi Novemba, 2025 hali ya ongezeko la Joto imeendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo nchini, ambapo hadi kufikia Novemba 27, 2025 kituo cha hali ya hewa cha Moshi (Kilimanjaro) kiliripoti kiwango cha juu zaidi cha nyuzi joto 35.7°C mnamo tarehe 21 Novemba, 2025 ikiwa ni ongezeko la nyuzi joto 4.2°C ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa mwezi Novemba katika kituo hicho.
Aidha,Kituo cha hali ya hewa cha Ilonga (Morogoro) kiliripoti nyuzi joto 35.5°C mnamo tarehe 20 Novemba (ongezeko la nyuzi joto 2.7°C). Kituo cha hali ya hewa Morogoro kiliripoti nyuzi joto 34.5°C mnamo tarehe 26 Novemba (ongezeko la nyuzi joto 2.3°C).
Pia,Kituo cha Ibadakuli (Shinyanga) kiliripoti nyuzi joto 33.6°C mnamo tarehe 14 Novemba (ongezeko la nyuzi joto 2.2°C), na Dar es salaam nyuzi joto 33.2 °C mnamo tarehe 19 na 21 Novemba (ongezeko la nyuzi joto 1.6°C).
TMA imebainisha kuwa, ongezeko la unyevu angani (Relative humidity) katika kipindi hiki linalosababishwa na mvuke wa Bahari hususan katika maeneo ya ukanda wa pwani na maeneo jirani limechangia pia mwili kuhisi joto zaidi ya viwango vinavyoripotiwa.
Hata hivyo, katika kipindi cha mwezi Desemba, 2025 vipindi vya mvua vinatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi nchini.
Hali hii inatarajiwa kusababisha kupungua kwa Joto katika baadhi ya maeneo hususan yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
"Kwa taarifa hii wananchi wanashauriwa kuendelea kuzingatia taarifa na tahadhari za hali mbaya ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania sambamba na kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazotokana na hali mbaya ya hewa."
Tags
Breaking News
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania
