Tujali utu wa Mtanzania-Dkt.Kijaji

NA SAIDI LUFUNE

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dk. Ashatu Kijaji (Mb), amewataka watumishi wa wizara na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo kuhakikisha wanazingatia maslahi na utu wa Mtanzania wanapotoa huduma kwa wananchi.
Dk. Kijaji ameyasema hayo jijini Dodoma mara baada ya kuripoti kazini na kufanya mazungumzo na menejimenti ya wizara, muda mfupi baada ya kuapishwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Amesema ni muhimu watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia utu na maslahi ya wananchi ili kuhakikisha wanapata huduma bora na maendeleo wanayostahili.

“Wananchi wanatuhitaji kwa yale tuliyoaminiwa kuyatekeleza kwa niaba ya Watanzania milioni 61. Ni jukumu letu kuwawezesha ili waendelee kuishi vizuri kama kawaida,” amesema Dk. Kijaji
Amefafanua kuwa, Ilani ya CCM imeweka mkazo katika ustawi wa watu, na ustawi huo hauwezi kupatikana endapo changamoto kama wanyamapori waharibifu hazitatatuliwa.

“Mkulima amelima ekari 20 za mbaazi, zimekomaa, halafu zinaharibiwa na tembo, ustawi haupo hapo. Hivyo lazima tufikirie mbali ili kulinda ustawi wao,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa falsafa ya Kazi na Utu ya Mhe. Rais inahitaji mtumishi kumweka mwananchi mbele: “unapomhudumia mtu, jiulize ungependa kuhudumiwa vivyo hivyo? Huo ndio msingi wa kazi yetu,”amesema Dk. Kijaji.
Waziri Kijaji pia ametoa wito kwa watumishi kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na mshikamano ili kutimiza ndoto za Watanzania kupitia sekta za uhifadhi, maliasili na utalii.

Aidha, amewapongeza kwa kazi wanayoifanya na kuhimiza kuendeleza ushirikiano ili kufikia malengo ya wizara.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mhe. Hamad Hassan Chande ameishukuru menejimenti na watumishi kwa mapokezi mazuri na kusisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa kuzingatia utu.

“Tumekuja kuungana nanyi katika ujenzi wa taifa. Hatukuja kama watawala, bali kama viongozi wa kutimiza ndoto ya Rais fanyeni kazi kwa utu, na mtambue thamani ya watu,” amesema Mhe. Chande.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hassan Abbas, ameahidi kutoa ushirikiano kwa uongozi mpya ili kufanikisha malengo ya wizara na serikali, hususan katika kuhudumia wananchi na kutangaza vivutio vya utalii.

Awali, Waziri Dk. Kijaji alikagua gwaride maalum lililoandaliwa na Jeshi la Uhifadhi (JU) akiongozwa na Katibu Mkuu, Dk. Abbas.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news