NA DIRAMAKINI
CHAMA cha Mawakili wa Serikali (PBA) kimempongeza Mheshimiwa Hamza Said Johari kufuatia uteuzi wake wa mara ya pili mfululizo kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa leo na chama hicho, kimeeleza kuwa uteuzi huo ni uthibitisho wa imani kubwa aliyopewa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Sambamba na ubobezi wa kitaaluma, uadilifu, na uzoefu wa muda mrefu alionao Mhe. Johari katika tasnia ya sheria na utumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Ibara ya 59 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni ya kikatiba, na uteuzi wake huzingatia sifa za kitaaluma na uzoefu wa kazi wa angalau miaka 15 katika masuala ya uwakili au usajili wa sheria.
Chama hicho kimebainisha kuwa, uteuzi wa aina hii si wa kisiasa, bali unatokana na weledi na uwezo wa kitaalamu.
“Ni muhimu kwa wananchi kutambua kwamba viongozi wanaoteuliwa kwa mujibu wa Katiba hupitia taratibu za kisheria na kiutendaji, hivyo taarifa zisizo sahihi kuhusu viongozi hawa zinaweza kuathiri heshima ya taasisi za umma na kupotosha jamii,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
PBA imesisitiza umuhimu wa wananchi kutafuta taarifa sahihi kutoka vyanzo rasmi kama vile Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali au tovuti za serikali kabla ya kusambaza au kuamini taarifa za mtandaoni.
Hamza Said Johari ni nani?
Mheshimiwa Johari ni Wakili namba moja nchini Tanzania kwa mujibu wa Sheria ya Mawakili, na ana uzoefu wa zaidi ya miaka 20 katika utumishi wa umma, hususan katika maeneo ya majadiliano ya mikataba, sheria za anga, sheria ya bahari na sheria za udhibiti.
Pia,ana Shahada ya Kwanza ya Sheria (LL.B) na Shahada ya Uzamili ya Sheria (LL.M) katika Sheria ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Kiev, Ukraine pamoja na Cheti cha Uongozi na Usimamizi kutoka Chuo cha Wafanyakazi wa Utawala cha India.
Aidha, amehudhuria mafunzo na semina nyingi za kitaaluma, na kuchapisha maandiko kadhaa kuhusu sheria za usafiri wa anga na bahari.
Katika uongozi wa kitaasisi, Mhe. Johari amewahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kipindi cha miaka tisa, Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Huduma za Anga (CANSO) kwa Kanda ya Afrika, na Mjumbe wa Kamati Tendaji ya CANSO kwa miaka sita.
Pia amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usafiri wa Anga ya SADC na Mwenyekiti wa Wakala wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (CASSOA).
Kwa sasa, mbali na majukumu yake kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Johari pia ni Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama,Mwenyekiti wa Jopo la Ithibati la Wasuluhishi, Wadadisi na Waamuzi,
Mwenyekiti wa Timu ya Wanasheria wa Serikali,Mjumbe wa Kamati ya Taifa ya Uendeshaji Uwekezaji, na Mjumbe wa Kamati ya Mawakili (The Advocates Committee).
Aidha, amewahi kuwa Mhadhiri Mgeni katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Mzumbe, na Chuo Kikuu cha Alexandria nchini Misri, akifundisha masomo ya Sheria za Kimataifa za Bahari na Usafirishaji.
Vilevile,Mheshimiwa Johari ameshiriki kama Mwenyekiti au Mpatanishi Kiongozi katika timu nyingi za majadiliano za Serikali, zikiwemo Migogoro ya mipaka kati ya Tanzania na nchi jirani (Malawi, Burundi, na Uganda);
Majadiliano ya mikataba ya huduma za anga kati ya Tanzania na mataifa zaidi ya 15, ikiwemo Marekani, Uingereza, China, na Falme za Kiarabu;
Majadiliano kuhusu makubaliano ya ubia na uwekezaji wa bandari, ikiwemo miradi na mikataba na DP World (UAE) na Bandari ya Adani (India).
Kwa mujibu wa Chama cha Mawakili wa Serikali, mafanikio haya yanadhihirisha uwezo wa juu wa kitaalamu na kizalendo wa Mheshimiwa Johari katika kulinda na kutetea maslahi ya taifa ndani na nje ya nchi.
Chama cha Mawakili wa Serikali kimepongeza uamuzi wa Serikali wa kumrejesha Mhe. Hamza Said Johari katika wadhifa huo muhimu, kikisisitiza kwamba uteuzi huo unaleta matumaini ya kuendeleza misingi ya utawala wa sheria, uwajibikaji na uadilifu katika utumishi wa umma.
“Tunampongeza kwa dhati Mheshimiwa Hamza Said Johari,Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali, na mfano wa kuigwa kwa mawakili wote nchini,”imeongeza taarifa hiyo.
Tags
Breaking News
Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania
Habari
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
PBA Tanzania




