NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kuwa, inatambua waandishi wa habari na vyombo vya habari nchini kama daraja muhimu la kufikia wananchi na wadau wengine ndani na nje ya nchi.

Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Dodoma, Dkt.Wilfred Mbowe ameyasema hayo Novemba 21,2025 jijini Dodoma wakati akifunga semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha.
Semina hiyo imeratibiwa na BoT huku ikiwaleta pamoja waandishi wa habari kutoka mikoa mitano ya Dodoma, Morogoro,Dar es Salaam, Zanzibar na Pwani.
"Yaani, bila waandishi wa habari na vyombo vya habari itakuwa vigumu sana kwa Benki Kuu kufikia malengo yake.Kufikia malengo na sera za Benki Kuu, wananchi wanatakiwa kupata taarifa za kina.
"Kuzipata kwa kina na kwa usahihi unaostahili ili waweze kufanya maamuzi sahihi katika mipango yao ya kiuchumi, kijamii sambamba na mwelekeo wa sera hizo."
Dkt.Mbowe amesema kuwa, semina hizo zinalenga pamoja na kutambua umahiri na ubobezi walionao waandishi wa habari kuwapa uelewa wa majukumu ya BoT na kupitia uelewa huo waweze kuelimisha umma.
Amesema, miongoni mwa mambo muhimu katika semina hizo ni kuwaelimisha kuhusu masuala yanayohusiana na mwelekeo wa sera ya fedha, fursa za kiuwekezaji, mageuzi katika sekta ya fedha.
Pia, maboresho katika mifumo ya malipo yanayolenga kupunguza gharama na kuongeza tija ili kuwezesha wananchi wengi zaidi kushiriki na kunufaika kupitia sekta ya fedha (Financial Inclusion).
Amesema, lengo la BoT ni kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa kina na kwa mapana zaidi,kwa wakati, kwa uelewa na kwa usahihi wa hali ya juu.
Vilevile ametoa rai kwa waandishi wa habari kuendelea kutumia kalamu zao kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia mfumo wa SEMA NA BoT ambao unawapa uwanda mpana wa kuwasiliana na BoT na kuwasilisha changamoto zao kutoka sekta ya fedha.

"Tunawashukuru sana waandishi na vyombo vya habari kwa ujumla wao nchini kwa kazi nzuri, pasipo habari zao, makala zao, matangazo yao, inawezekana kabisa Benki Kuu isingefikia mafanikio ambayo inajivunia leo na baadhi ya mafanikio hayo ni kuweka utulivu wa bei, utulivu wa shilingi yetu, kujenga sekta ya fedha na mifumo ya malipo iliyo imara, tulivu, kuaminika,jumuishi na zaidi kabisa taarifa zake kuwafikia wananchi kwa wingi."
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Dodoma, Dkt.Wilfred Mbowe amewahimiza waandishi wa habari nchini kuendelea kutumia kalamu zao kuhabarisha umma kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Mathalani, kwa Jiji la Dodoma amesema, Serikali itatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo Mji wa Serikali Mtumba, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato.
Miradi mingine amesema ni Mradi wa Kuinua Vijana Kiuchumi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT),Barabara ya lami ya njia nne ya Mzunguko (Outer Ring Road) ndani ya Jiji la Dodoma,reli ya kisasa na mingineyo.
Amesema, wananchi wanahitaji kuifahamu miradi hiyo kwa kina kupitia kalamu za waandishi wa habari nchini ili wananchi wajue Serikali yao inafanya nini,wapi na miradi imefikia hatua gani.
"Miradi hiyo inahakisi kazi kubwa inayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan."
