DODOMA-Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limemthibitisha Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba kuwa Waziri Mkuu mpya wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika kikao kilichofanyika leo Novemba 13, 2025, katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma.
Dkt. Nchemba aliyekuwa Waziri wa Fedha katika Serikali ya Awamu ya Sita, amepata kura 369 za ndiyo kati ya kura 371 zilizopigwa na wabunge, huku kura mbili zikiharibika.
Akizungumza mara baada ya kuthibitishwa, Dkt. Nchemba amesema kuwa Serikali anayoiongoza itakuwa ya wananchi wote na haitabagua mtu kwa misingi yoyote.
Amesema kuwa kila Mtanzania atapata haki ya kusikilizwa katika ofisi za umma, akibainisha kuwa anatambua changamoto wanazopitia wananchi wa hali ya chini kutokana na uzoefu wake binafsi wa maisha magumu baada ya kumaliza chuo.
Amesema kuwa alishawahi kufanya kazi ya kubeba zege na matofali ili kujipatia kipato, na hivyo anaelewa maumivu ya vijana wasio na ajira.
Pia,ameahidi kwamba Serikali itatekeleza dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutengeneza ajira milioni nane kwa vijana nchini, kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi.
Aidha, Dkt. Nchemba amebainisha kuwa utendaji wa Serikali utajikita katika kutatua matatizo ya wananchi kwa matokeo ya haraka, sambamba na kusimamia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Amesema kuwa, dira hiyo imebeba matumaini makubwa kwa Watanzania, hasa vijana, na kwamba awamu hii ya pili ya Serikali ya Awamu ya Sita itaanza utekelezaji wake rasmi.
Amebainisha kuwa Serikali itaendelea kuboresha huduma za kijamii kwa kuendeleza miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita chini ya Rais Samia, ikiwemo ujenzi wa shule, hospitali, vituo vya afya na miradi ya umeme vijijini.
Amesema kuwa, hatua hizo ni kielelezo cha Serikali inayoweka kipaumbele katika maisha ya wananchi, huku akiahidi kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora katika maeneo yote ya nchi.
Pia, amesema kuwa, atasimamia kwa bidii, uaminifu na uwajibikaji mkubwa majukumu yake kama Waziri Mkuu, akisisitiza kuwa Serikali yake itakuwa ya ushirikiano, inayoweka mbele maslahi ya wananchi wote bila ubaguzi.
Kuhusu Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba
Dkt.Nchemba anajulikana kama mfano wa mafanikio yanayotokana na bidii na kujituma. Alikulia katika mazingira ya kijijini na alitoka katika familia yenye hali ya kawaida, ambapo aliwahi kuchunga ng'ombe nyikani akiwa kijana mdogo.
Maisha hayo yalimfundisha nidhamu, uvumilivu na kuthamini kazi halali. Mara kadhaa amekuwa akisimulia hadithi ya maisha yake kama njia ya kuwahamasisha vijana kupambana kupitia elimu na kujituma.
Alisoma shule ya msingi Makunda mkoani Singida kati ya mwaka 1987 hadi 1993, kisha akaendelea na masomo ya sekondari katika shule ya sekondari Ilboru mkoani Arusha na sekondari ya Mazengo mkoani Dodoma ngazi ya kidato cha tano na sita.
Baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisomea shahada ya kwanza ya uchumi na baadaye akahitimu shahada ya uzamili mwaka 2006, na baadaye kupata shahada ya uzamivu kutoka chuo hicho hicho.
Safari yake ya kisiasa ilianza kupanda kasi mwaka 2010 aliposhinda ubunge wa Jimbo la Iramba Magharibi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alirudi tena bungeni mwaka 2015. Ndani ya chama chake amejipatia heshima kama kiongozi mwenye msimamo thabiti na anayejali nidhamu katika utumishi wa umma.
Amewahi kuwa Katibu Mkuu Msaidizi, mjumbe wa Kamati Kuu, Halmashauri Kuu na sekretarieti ya chama kwa miaka mingi.
Dkt. Mwigulu amewahi kushika nafasi mbalimbali serikalini. Alianza kama Naibu Waziri wa Fedha katika serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi mwaka 2015, kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2016.
Mwaka 2021 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, nafasi aliyoishikilia hadi uteuzi wake kuwa Waziri Mkuu.
Mwigulu ni mtu anayejulikana kwa uzalendo wake. Mara nyingi huonekana akiwa amevalia skafu yenye rangi za bendera ya taifa, akisisitiza umuhimu wa kuipenda Tanzania.
Pia amekuwa akisaidia vijana hasa katika masuala ya elimu, akiamini kuwa elimu ndiyo njia kuu ya kupambana na umasikini.
Uteuzi wake kuwa Waziri Mkuu uliwashangaza watu wengi, kwani jina lake halikuelezwa sana katika mijadala ya awali.
Wakati wa uteuzi huo, majina kama ya Dk. Tulia Ackson, Paul Makonda, Profesa Kitila Mkumbo na Dotto Biteko ndiyo yalikuwa yakitajwa zaidi.
Hata hivyo, Rais alimteua Mwigulu kutokana na uzoefu wake serikalini na uwezo wake wa kuongoza shughuli za serikali bungeni kwa ufanisi.
Nchemba anakuwa Waziri Mkuu wa 12 wa Tanzania, akifuata nyayo za Mawaziri wengine Wakuu Tanzania, Julius Kambarage Nyerere 1960-1962, Rashidi Kawawa 1962–1962 na tena 1972–1977, Edward Moringe Sokoine 1977-1980 na 1983-1984 na Cleopa David Msuya 1980–1983 na tena 1994-1995.
Wengine ni Salim Ahmed Salim 1984–1985, Joseph Sinde Warioba 1985–1990, John Malecela 1990-1994, Frederick Sumaye 1995-2005, Edward Lowassa 2005-2008, Mizengo Pinda 2008–2015 na Kassim Majaliwa 2015-2025, anayemaliza muda wake sasa.
