Yanga SC kuingia Zanzibar tayari kuikabili FAR Rabat

DAR-Kikosi cha Yanga SC kinatarajiwa kuelekea Zanzibar kesho kwa ajili ya mchezo wa Ligi ya Mabingwa barani Afrika dhidi ya FAR Rabat, utakaopigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex Jumamosi hii.

Kwa mujibu wa Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ally Kamwe, timu itaondoka Dar es Salaam saa tatu asubuhi kwa kutumia usafiri wa boti.

Kamwe amesema,baadhi ya wachezaji akiwemo Prince Dube, Celestine Ecua na Lassine Kouma ambao bado wako kwenye majukumu ya timu zao za taifa hawataungana na msafara wa kesho.
Hata hivyo, uongozi wa Yanga tayari umeweka utaratibu utakaowawezesha kuungana na wenzao moja kwa moja visiwani Zanzibar mara tu watakapomaliza majukumu yao.

Aidha, wachezaji waliokuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars wamesharejea na watakuwa sehemu ya safari ya kesho.

Kamwe amewataka mashabiki wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi kuipokea timu, akisema mchezo huo ni wa kihistoria kwa kuwa unazikutanisha timu mbili bora barani Afrika kwa sasa.

Katika hatua nyingine, Kamwe ametangaza kuwa jezi mpya za Yanga kwa ajili ya kampeni za Ligi ya Mabingwa zitazinduliwa na kuanza kuuzwa Alhamisi hii.

Amesisitiza kuwa, jezi hizo ni maalumu kwa michuano ya kimataifa, hivyo idadi yake haitakuwa kubwa. “Nawakumbusha wanachama na mashabiki kuhakikisha wanazipata mapema. Jezi hizi ni za viwango vya juu sana,” amesema.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya mchezo wenyewe, Kamwe ameeleza kuwa mechi dhidi ya FAR Rabat ndiyo itakayoshikilia rekodi kama mchezo mkubwa zaidi kuwahi kuchezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex.

Kwa mujibu wake, mchezo huo ndio unaovuta hisia na mijadala mingi zaidi barani Afrika kwa sasa.

Ameongeza kuwa, tiketi za mchezo huo zimeanza kuuzwa katika vituo mbalimbali pamoja na kwa njia ya mtandao.

Kwa mashabiki waliopo Zanzibar, kadi za zamani zitaendelea kutumika, na kwa waliopoteza kadi, utaratibu wa kupata mpya utawekwa nje ya uwanja kesho.

Kamwe amesisitiza kuwa muda wa maneno umeisha na sasa ni wakati wa vitendo.

“Tunakwenda kupambana na FAR Rabat kupata pointi tatu. Tumeyasikia maneno yote yaliyosemwa dhidi yetu,majibu yetu yatakuwa uwanjani,”amesema.

Pia,amewataka wana Yanga kujiandaa kikamilifu kwa wiki hii ya kazi na kuhakikisha hawakosi burudani ya kipekee Jumamosi kwenye Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Zanzibar.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here