NA DIRAMAKINI
UONGOZI wa Klabu ya Yanga umetangaza kuwa utatumia uwanja wa New Amaan Complex, kama uwanja wao wa michezo ya nyumbani kwenye hatua ya makundi katika michuano ya Klabu Bingwa barani Afrika.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 5,2025 na Afisa Habari wa Klabu hiyo Ally Kamwe alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Baada ya uongozi kufanya Tathimini na kuangalia maslahi mapana ya Klabu yetu, nipende kuwatangazia kuwa mechi zetu zote 3 za nyumbani kwenye hatua ya Makundi, tutatumia uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
“Niwaombe sana mashabiki na Wanachama wetu kutoka visiwa vya Pemba na Unguja kujiandaa kuipokea timu na maandalizi ya nguvu kuelekea mchezo wa kwanza wa nyumbani dhidi ya FAR RABAT.
“Wanachama wengine kutoka mikoani tujiandae pia, tupo kwenye kundi gumu lakini tukiwa wamoja, tukiendelea kushiriana kwa umoja wetu tutatoboa."
Kuhusu Clement Mzize amesema kuwa,“Mara ya mwisho tuliwajulisha kuhusu hali ya majeraha ya mchezaji Clement Mzize. Baada ya ushauri wa jopo la madaktari wakishirikiana na benchi la Ufundi na Mchezaji mwenyewe tulikubaliana afanyiwe upasuaji.
“Maamuzi haya yalikuja baada ya kuona anaendelea kupata maumivu kwenye goti lake kila alipokuwa akirejea uwanjani. Nipende kuutangazia Umma kuwa, mchezaji Clement Mzize atakuwa nje ya uwanja kwa wiki nane mpaka kumi,”amesema Ally Kamwe.
Ameongeza kuwa, "Kikosi chetu kimerejea kambini hapo jana na tayari imeanza maandalizi ya mchezo wa ligi ya NBC ambao utafanyika tarehe 9 dhidi ya KMC katika uwanja wa KMC Mwenge Dar Es Salaam.
"Kuhusu mchezo wetu dhidi ya Prisons SC uliyopangwa kuchezwa Dodoma umeahirishwa na tunasubiri tarehe mpya itakayopangwa na Bodi ya Ligi."
